Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro ameomba msamaha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kwa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka.

Julai mwaka jana, Muro alifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF dhidi yake.

Katika barua yake kwa TFF, Muro amesema kwamba anakiri kupata barua ya kufungiwa kutoka Kamati ya Maadili, lakini anaomba msamaha baada ya kutumikia nusu ya adhabu yake.

Muro ameomba apunguziwe adhabu na kurudi kutekeleza majukumu yake kwa mwajirin wake, Yanga SC kuanzia kipindi hiki cha michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayoendelea visiwani Zanzibar.

Mapema wiki iliyopita, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa mahasimu, Simba SC, Hajji Manara alimuombea msamaha Muro pia. Na Wasemaji wa timu nyingine akiwemo Massau Bwire wa Ruvu Shooting walkimuombea msamaha pia mwenzao huyo, wakiamini atakuwa amejirekebisha.

Muro alifungiwa Julai 8 mwaka jana baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam.

Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.

Kwa kosa hilo akahukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja- wakati shitaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.

Mbeya City Waivutia Kasi Azam FC, Kwenda Sumbawanga
Mbora Wa Wabora Afrika Kujulikana Leo