Saa chache kabla ya mtanange mzito dhidi ya Al Ahly ya Misri, Yanga imejigamba kuichapa timu hiyo kama sehemu ya kulipiza kisasi cha ndugu zao Azam FC ambao walichezea kichapo cha 3-0 na kutoka kwa Espérance De Tunis.

Muro

Msemaji wa Yanga, Jerry Muro ambaye ameambatana na timu hiyo nchini Misri wakisubiri dakika chache kujua mbivu na mbichi katika uwanja wa Jeshi wa Borg El Arab, amesema kuwa kichapo cha Azam FC cha jana usiku kiliwavunja moyo kiasi fulani lakini wamerudisha morali na sasa wamedhamiri kuichapa Al Ahly.

Akiongea na Radio One Stereo jioni hii, Muro amesisitiza kuwa leo lazima Yanga itashinda na kuishangaza dunia.

“Tayari wenzetu wameshatoka. Kwahiyo hii kwetu inamaanisha kwamba tuna kila sababu ya kuhakikisha tunasonga mbele kwenye michuano hii kwa gharama yoyote. Sisi tunachotaka leo ni kulipa kisasi cha ndugu zetu  na jukumu letu ni kuhakikisha pale wanapotereza wenzetu sisi tunapasawazisha na tunasonga mbele kuiletea heshima nchi yetu na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Muro.

“Naomba niwahakikishie mashabiki kwamba wakati wowote kuanzia sasa kikosi kinaingia uwanjani. Mimi nawaambia wasijali, leo tuna kila sababu ya kuwatoa kimasomaso Watanzania. Na leo tunakenda kufanya, kwa njia yoyote ile Mwarabu lazima apigwe,” alisisitiza.

Yanga wanahitaji ushindi au sare ya magoli kuanzia 2-2 ili kuwawezesha kuvuka hatua ya 16 Bora.

Amfanyia unyama huu kijana aliyembaka mwanae mwenye umri wa miezi 7
Mahakama yafuta Sheria ya ‘matumizi mabaya ya mtandao na vifaa vya mawasiliano’