Jeshi la Polisi Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya (ADU) limewakamata Abdallah Chande na Crispian Ochanda wakazi wa Tegeta Ununio Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa na heroin zenye uzito wa kilo 7.73.

Mkuu wa kitengo cha ADU, Kabaleke Hassan leo Juni 16, 2021 amesema Juni 10, 2021 saa 12 asubuhi maeneo ya Tegeta Abdallah Chande alikamatwa na alipohojiwa alikiri kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kwamba alikuwa amezificha kwa Crispian Ochanda.

Mkuu wa kitengo Hassan amesema kuwa mtuhumiwa huyo aliwaongoza askari hadi kwa Ochanda na walipofika walimkuta na dawa hizo pamoja na bangi zenye uzito wa gramu 2.94 zilizokuwa kwenye gari.

“Aprili 29, 2021 maeneo ya Sangasanga Check Point mkoani Morogoro tuliwakamata watu 10 wakiwa na heroin kilo 20.24 wakiwa wanazisafirisha kwenda jijini Dar es Salaam tukabaini kuna watu wameandaliwa kuzipokea na kuzisambaza hadi Tanga ambao alikuwa Ally Juma na Chande  ambao wote walikuwa  maeneo ya Chalinze mkoani Pwani.”

“Wakati wanamkamata  Juma mtuhumiwa Chande alifanikiwa kuwatoroka askari polisi kabla ya kukamatwa hivyo tuliendelea kumtafuta ili aunganishwe na wenzake 10 ndipo tukabaini yupo maeneo ya Tegeta Ununio ndipo Juni 10 mwaka huu tukamkamata,” amesema Hassan.

Rais Samia ateua Wenyeviti wa Bodi, Anne Makinda astaafu
Tanzania, Marekani kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza