Jeshi la Polisi limepiga marufuku kufanyika kwa maandamano yaliyoitishwa na viongozi wa Chadema yenye lengo la kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu, maandamano ambayo yanakusudiwa ‘kutokuwa na kikomo’.

Akitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema kuwa Jeshi hilo limepiga marufuku maandamano hayo kutokana na athari kubwa hasa za kiuchumi ambazo zinaweza kusababishwa na maandamano hayo.

Alisema kuwa maandamano yatasababisha usumbufu kwa wafanyakazi wadogo kwa kulazimisha shughuli za kawaida kusimama kwa muda ambao haujulikani huku suala la amani likiwa katika utata.

Aidha, Kamanda Kova alisema kuwa jeshi la polisi halitaweza kuongoza maandamano ya mlengo huo kwa kuwa endapo itajihusisha na ulinzi wa maandamano hayo ya bila kikomo, hii itamaanisha kuwa Jeshi la Polisi litaacha kazi nyingine zote na kulinda maandamano hayo usiku na mchana.

Kamanda Kova aliwataka wananchi kuendelea na kazi zao za kila siku na kutoshiriki katika maandamano hayo huku akieleza kuwa yatashusha vipato vya wananchi masikini kwani hawatakuwa na uwezo wa kufanya kazi na biashara zao.

'Hello' ya Adele Yavunja Rekodi Nyingine
Wanafunzi Walia Na Bodi Ya Mikopo, Bodi Yatoa Ufafanuzi