Jeshi la Polisi nchini Uganda limeomba msamaha baada ya askari wake kuonekana kwenye mkanda wa video wakimpiga mwandishi wa habari ambaye alikuwa akitimiza wajibu wake kwenye maandamano ya kushutumu kukamatwa kwa mbunge Bobi Wine.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imeeleza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na askari wake si cha weledi na kusema kuwa watakamatwa kwa mujibu wa sheria za jeshi nchini humo.

Katika video iliyorushwa mtandaoni, ilimuonyesha mwandishi wa habari wa shirika la Reuters, James Akena akipigwa kwa fimbo na askari wawili jijini Kampala.

Aidha, Kumekuwa na mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Uganda baada ya mbunge Bobi Wine na wabunge wanne wa upinzani kukamatwa wiki iliyopita.

Kwa upande wake, Bobi Wine ambaye ni mbunge maarufu nchini Uganda amefanikiwa kuteka umma nchini humo huku akiungwa mkono na asilimia kubwa ya vijana, kwa kuendesha harakati za kisiasa dhidi ya Raisi Yoweri Kaguta Museveni.

Mwanasheria wa Trump aburuzwa mahakamani
BASATA yawanyooshea kidole wasanii