Mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa Profesa Ibrahim Lipumba uliotakiwa kuanza leo Jumanne Machi 12, 2019 katika Hoteli ya Lekam Buguruni umezuiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala jijini Dar es Salaam ametoa zuio hilo baada ya kufika eneo la mkutano na kueleza kuwa. “Tumekuja kuwaeleza kuhusu zuio hili kwa sababu wameshalipeleka makao makuu ya Polisi,” amesema Chembera.

Aidha, Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Thomas Malima na Naibu Katibu mkuu (Bara) Magdalena Sakaya wamesema hawajapata katazo hilo kwa hiyo wataendelea na mkutano. “Sisi hatujapata hilo katazo, tunaendelea na mkutano,” amesema Malima.

Awali, akizungumzia na waandishi wa habari, mkurugenzi wa uhusiano wa chama hicho, Abdul Kambaya amesema katazo la Mahakama limewataja watu watatu akiwemo Profesa Lipumba na Magdalena Sakaya.

Kambaya amesema kuwa waliowekewa katazo watashiriki katika mkutano huo kama waalikwa tu. “Katazo limewataja watu watatu, mkutano mkuu unaitishwa na Baraza Kuu, wao watakuja kama waalikwa tu,”

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tovuti ya Mwananchi imeeleza kuwa, licha ya katazo la Polisi lakini mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba aliingia katika eneo la mkutano na kupokelewa kwa shangwe huku akiingizwa kwenye ukumbi mara tu baada ya RPC wa Ilala kuondoka eneo hilo, huku waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika mkutano huo.

Mkutano huo ambao waandishi wa habari hawaruhusiwi kuingia ukumbini unaendelea ukipata baraka za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa, ambapo Naibu Msajili, Sisty Nyahoza ndiye aliyeufungua kwa kutoa hotuba.

Amesema mkutano huo unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndio maana umetambuliwa na Ofisi yake.

Amewapongeza kwa kile alichosema wamehimili mapito ya mahakama na wameendelea kukilinda chama, pia kwa kuweza kuteua bodi mpya ya wadhamini na kuwakumbusha wajibu wao wa kutunza Mali na fedha. Amewataka pia kuzingatia mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.

Nyahoza pia amesema sheria ya sasa ya vyama vya siasa hairuhusu vyama kuwa na vikundi vya ulinzi.

Aidha, licha ya RPC wa Ilala, Zubery Chembera aliyeleta taarifa ya zuio, Askari wa jeshi hilo wameendelea kubaki eneo hilo wakiendelea na ulinzi.

Kisiwa cha Lamu chapiga marufuku matumizi ya Magari, Punda pekee kutumika
Wafanyabiashara Kibaha wazuia msafara wa Waziri Jafo