Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limeanza kutekeleza agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli la kusafirisha korosho kutoka Mikoa ya Kusini.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi hilo, Meja Gaudence Ilonda, magari 70 yameanza safari leo kutoka kikosi cha usafirishaji kwenye kambi ya Mgulani jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufuata mzigo huo.

“Oparesheni Korosho kama mlivyosikia ni tamko la Mheshimiwa Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, na sisi kama Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tuko tayari. Tumeanza kutekeleza jukumu hilo tangu jana, magari yameanza kuondoka,” alisema Meja Ilonda.

Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama wa maghala ya korosho katika Mikoa ya Kusini, alisema kuwa ulinzi umeimarishwa na hakuna mtu anayeweza kuchezea eneo hilo.

“Kuna askari wa kutosha ambao wamemwagwa katika eneo la Mtwara tayari kwa kukabili shughuli ya usafirishaji,” alisema.

Naye Mkuu wa kikosi hicho, Luteni Kanal Elias Kyejo alisema kuwa kazi wanaoyoenda kuifanya katika maeneo hayo itafanyika kwa weledi kwani lengo ni kulinda na kuhakikisha maagizo ya Rais yanaenda vizuri.

Video: BMT yatuma salamu kwa wenyeviti wa riadha wa mikoa
Chadema watetea hatua ya mbunge wao kuingia na Ilani ya CCM Bungeni

Comments

comments