Wanasema mambo yakienda kombo yaache usiende nayo, lakini nidhamu na maadili vikienda kombo vinahitaji jicho la tatu kuviangalia na kutafuta utatuzi wa kudumu bila kuelemewa na hisia pekee na masikitiko mazito!

Nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa nasikia mara kadhaa bibi yangu ambaye hivi sasa ni marehemu akipinga kwa nguvu zote adhabu ambazo binamu yangu alikuwa anatupatia kutokana na makosa tuliyokuwa tunayafanya.

Nilimshudia bibi akizila kula chakula kwa madai kuwa ‘utumbo umejikunja’ kwasababu yeye ni mzazi. Hii ilitokana na kushuhudia adhabu ya  mvua ya viboko kwenye makalio yetu, nilikuwa mimi na dada yangu ambao kweli tulikuwa watukutu kiasi cha kupewa jina la kilugha ‘tamakwigwa’, yaani wasiosikia.

Hata hivyo, adhabu hizo zilitujengea hofu zaidi lakini sio utii na nidhamu. Tuliendelea kufanya matukio kwa kujificha na tuliharibu mengi.

Vipigo vilitupa nidhamu ya uoga tu, hadi alipobadili mbinu za ufundishaji na kutugeuzia katika mafunzo ya dini kwa nguvu zaidi, hapo tulianza kunywea na kuvaa nidhamu kamili taratibu kila tulipofunzwa kumcha Mungu. Alitupika kisaikolojia na kiroho, alitufunza kuimba nyimbo nzuri za dini, ilikuwa njia rafiki zaidi.

Lakini binadamu yetu huyo pomoja na yote hakuiweka mbali fimbo yake, alisema hata Biblia Takatifu inasema ‘usimnyime mtoto mapigo’. Duh!

Nimeyakumbuka hayo kutokana na tukio la juzi ambapo ilisambaa video inayowaonesha ‘majambazi’ wakimshambulia mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari ya kutwa ya Mbeya, Sebastian Chinguku.

Niwie radhi kwa kutumia neno ‘majambazi’, kiuhalisia wale ni walimu-wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo shuleni hapo. Lakini nimetumia neno hilo nikimnukuu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu nchemba aliyepata hasira kama ilivyokuwa kwa kila mwenye akili timamu aliyeiangalia video hiyo.

“This is real sad. Nimewatuma watu wangu wa mtandao walocate tukio lilipotokea na kuwakamata hao majambazi. Maana mwalimu hawezi kuwa na ukatili wa kijambazi namna hiyo,” Waziri Nchemba aliandika mtandaoni.

picha-ya-adhabu-walimu

Kwakweli haijalishi ni kosa gani alilolifanya yule mwanafunzi, hakuna kinachoweza kuwapa uhalali walimu wale kufanya unyama kiasi kile. Kwa sisi wazazi ambao tuna moyo kama wa bibi yangu, hatukuweza kuangalia kwa kurudiarudia ile video kwakuwa utumbo unajikunja. Inaumiza sana.

Kutokana na uzito wa tukio hilo baya na jinsi lilivyosambaa, Serikali ilisimama na kuchukua hatua madhubuti. Mawaziri watatu walitoa tamko na maamuzi ndani ya siku moja. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliagiza wakamatwe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako aliagiza wafukuzwe vyuoni na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene aliagiza Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuvuliwa madaraka.

Ninapongeza kwa moyo wa dhati hatua zilizochukuliwa na jinsi jamii ilivyotoa mrejesho wake mkubwa kupinga na kulaani kitendo hiki.

Lakini, kuna haja pia ya kuangalia upande wa pili wa barabara ambako kuna tatizo kubwa zaidi. Tusiishie kutatua ‘tukio’, tuwaze namna ya kutatua jambo/suala (issue). Msomi mmoja, Kendra Cherry aliwahi kusema “utatuzi wa tatizo ni mchakato wa kiakili au kisaikolojia na sio tukio tu”.

Masikitiko yetu juu ya video tuliyoiona iliyotukunja utumbo sisi wazazi, isitufanye vipofu wa kuangalia upande wa pili wa barabara na badala yake kubaki na masikitiko tu.

Nidhamu kwa wanafunzi wa shule nyingi hasa za Serikali iko katika kiwango cha kutisha na walimu wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana wakiteswa kisaikolojia na wanafunzi.

Kama tulivyowashangaa walimu wale tukiwafananisha na majambazi, baadhi ya wanafunzi ambao ni watoto wetu sisi wenyewe, wakifika shuleni hugeuka kuwa vibaka wa kutisha wenye sura ya huruma wauonapo umma pale wanapobainika.

Kwa mfano, wiki hii kuna video imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwanonesha wanafunzi wa kike na mmoja wa kiume, wote wa kidato cha tatu, waliokamatwa na walimu wao wakitumia madawa ya kulevya aina ya bangi na pombe kali aina ya viroba. Hii inatisha!

Ukiwaangalia, sura zao zinatia huruma, ni watoto wadogo ambao ukiambiwa wameonewa utakubali haraka sana. Hawafanani kabisa na wavuta bangi au wanywa viroba. Lakini ndio uhalisia ambao wazazi wao hawaujui kabisa na daima wanaweza kusimama wakawatetea mbele ya mbingu.

Mwalimu mmoja wa Sekondari jijini Mwanza, ni rafiki yangu nilisoma naye chuoni, ameniambia kuwa yeye aliwahi kutekwa na wanafunzi wake wa kidato cha nne, wakamkalisha chini na wakampa onyo kali. “Wale ni watoto wa mtaani, ukiwafuatilia zaidi ya hapo watakufanya vibaya huko mtaani,” aliniambia na kuongeza kuwa hakutaka kusema popote akihofia.

Binafsi niliwahi kushuhudia mwanafunzi wa kidato cha tano wa shule moja ya bweni akimwagia mwalimu uji kwa hasira. Bahati nzuri uji ule haukuwa wa moto sana. Lakini kwa busara za mwalimu mkuu alilibeba jambo lile na mwanafunzi huyo mbabe alimaliza kidato cha sita.

Hiyo ni mifano michache tu, wote tuliwahi kuwa wanafunzi tunayo mifano halisi mingi sana, jaribu kuwaza tu hata kama ulisoma Seminari ambako kuna sheria ngumu sana, kuna kitu uliona. Baadhi ya wanafunzi wa Seminari tulikuwa tunakutana nao ‘Club’, wametoroka usiku na wanarudi usiku, asubuhi wanaingia kanisani kabla ya darasa! Na wanachukua namba zetu za simu, ina maana wana simu bwenini?

Tatizo la wanafunzi kutumia mihadarati mashuleni lipo hadi katika shule za msingi ambapo liliwahi kujadiliwa hasa kutokana na watoto kupewa zawadi za pipi na vitu vingine. Mihadarati hiyo hutengeneza tatizo kubwa la kuporomoka kwa maadili.

Ingawa inaweza kuonekana kuwa kuna uadui hivi kati ya baadhi ya walimu na wanafunzi wao, upo ‘utovu wa nidhamu shirikishi’ mashuleni ambapo pia ni hatari sana. Yaani mwalimu na mwanafunzi wanashirikiana kufanya jambo baya. Hii ni sawa na polisi kushirikiana na mwizi kufanya uhalifu. Baadhi ya walimu huanzisha urafiki wa karibu na wanafunzi na kufichiana siri za uharibifu wanaoufanya. Unaweza kudhani mambo ni shwari kwakuwa hakuna mgorogoro, kumbe ni hatari zaidi kwakuwa mlinzi na mwizi lao moja.

Yote kwa yote, naiomba Serikali ishirikiane kwa karibu na walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kumulika mfumo wa elimu utakaojenga nidhamu na maadili mema bila kunyoosheana vidole kwenye matukio. Matukio ni matokeo ya jambo/suala. Tutafute njia ya kutatua tatizo ili kuepuka matukio.

katuni-ya-mwalimu-mkuu

Kwa wazazi, maadili na nidhamu zijengwe kuanzia katika ngazi ya familia, sio kuanzia shuleni. Kama msingi wa familia utakua imara kimaadili, hata hatutakuwa na walimu majambazi wala wanafunzi vibaka.

Tahadhari yangu ni kwamba, kutokana na tukio la Mbeya, hivi sasa imejengeka taswira kwa baadhi ya watu kuwa wanafunzi wanaonewa sana na walimu ni wakatili. Mtazamo huu wa jumla ambao ni hasi unaweza kuzua tatizo jingine kama lile la madaktari ambalo lilipelekea ndugu wa mgonjwa kumpiga daktari.

Tutafute njia mahususi ya kukomesha ukatili mashuleni, hata kama ni kuondoa kabisa adhabu ya viboko, lakini tuwe na mfumo mzuri wa kujenga nidhamu na utii kwa wanafunzi na kizazi chetu. Tukizingatia hilo, wanafunzi wote watawaheshimu walimu wao, walimu wote watawapenda wanafunzi na kufuata maadili ya kazi zao.

*Elimu bila nidhamu na maadili ni BOMU.

Ndugai afumua Kamati ya Bunge na kuisuka upya
#MdahaloUrais: Trump asema angekuwa Rais Clinton angekuwa jela, clinton aomba radhi lakini…