Ni mara ngapi umetuma CV kwa mwajiri na hata kujibiwa hujajibiwa?

Tatizo inaweza ikawa sio kwamba huna ujuzi wa kutosha, bali ni kwamba kuna ushindani mkubwa sana Tanzania.

Zaidi ya asilimia 10 ya watu nchini wamekosa ajira na makampuni hupokea wastani wa maombi 100 ya kazi kwa tangazo moja la kazi. Hivyo, CV yako lazima ijitokeze vizuri. Utaratibu wa kuomba kazi unaweza ukawa tofauti kati ya makampuni na mashirika, ila yote yatahitaji uwatumie CV.

Sasa, unaweza ukafanyaje kufanya CV yako ijitokeze vizuri zaidi ya nyingine?

Kwa kuwa sisi ni rasilimali kubwa zaidi nchini kwa waajiri kutafuta wanaotafuta kazi, kadri miaka inavyokwenda tumeweza kujua siri za kuandika CV safi na tutawaambia siri hizo sasa hivi.

Haswa, CV ni nini?

CV ni maelezo ya ujumla kwa kiundani ya historia yako ya kazi na shule. Kwa kawaida, inatumika kwenye maombi ya kazi ya nafasi za kati, za juu na za utafiti.

Sasa, vidokezo vifuatayo vitasaidia kufanya CV yako iwe bora na hivyo, kukusaidia kupata usaili.

Kuwa na mpango

“Kushindwa kuwa na mpango ni mpango wa kushindwa” – Benjamin Franklin

Unakumbuka shuleni tulifundishwa kupanga insha zetu kabla ya kuziandika? Basi, kuandika CV ni vilevile. Kabla ya kuiandika inabidi ufanye vifuatayo:

  1. Soma na kuelewa maelezo ya kazi

Una ujuzi gani? Mwajiri anatafuta mfanyakazi wa aina gani? Maswali haya ni muhimu kujua kama utaiweza hiyo kazi au la. Pia, ni vizuri kujua nini hasa ni muhimu kwa muajiri na kufanya maombi yako yaendane zaidi na mahitaji ya mwajiri.

Kwa mfano, kama kazi inaweka umuhimu kwenye ujuzi wa kutumia mitandao ya kijamii kwa matangazo, hakikisha CV yako ina kazi zote zilizohitaji matumizi ya mitandao ya kijamii.

  1. Andika maneno muhimu yaliyotumika kwenye maelezo ya kazi, uyatumie kwenye CV

Usichukue sentensi nzima kutoka kwenye maelezo ya kazi na ukaitumia vile vile kwenye CV yako. Ila, tumia lugha na baadhi ya maneno yaliyotumika kwenye CV yako.

Kwa mfano: Mitandao ya kijamii, ujuzi bora wa utafiti.

  1. Fanya utafiti juu ya kampuni iliyotangaza kazi

Pamoja na kuchambua maelezo ya kazi, ni muhimu kufanya utafiti juu ya kampuni yenyewe. Kama wana tovuti au wapo kwenye mitandao ya kijamii, jaribu kujua ni kazi gani na sekta ipi wanayohusika nayo. Pia, ikiwezekana jaribu kuwajua wafanyakazi/meneja wa kampuni hiyo. Hii itakusaidia kujua maadili na muelekeo wa kampuni. Pia, itakusaidia kuweka maombi yako ya kazi yaendane na mahitaji ya kampuni hiyo.

  1. Orodhesha ujuzi wako wa kufanya kazi

Hapa, usiweke kazi zote ulizozifanya maishani mwako ila, weka zile ambazo zilikuongezea ujuzi utakayo kusaidia kufanya kazi unayoomba.

Andika

Staili inayotumika zaidi kwenye kuandika CV ni ifuatayo:

  1. Lengo la CV na ujuzi wako
  2. Ujuzi wako wa kazi
  3. Mafanikio maalum
  4. Elimu
  5. Ujuzi muhimu binafsi

Business Insider wanasema kwamba kwa wastani, mwajiri anaangalia CV kwa sekunde 6 tu kabla ya kuamua kama mtafuta ajira anafaa au hafai. Kwa hiyo, hakikisha kwamba:

1 – Zingatia staili

  • Tumia maandishi ya kawaida ya Times New Roman
  • Tumia size 9 – 12 ya herufi
  • Hakikisha unatumia staili moja ya kuandaa CV nzima

2 – Hakikisha ni rahisi kusomeka na kueleweka

  • CV isiwe zaidi ya ukursasa 2
  • Usitumie sentensi ndefu

Fikiria msomaji

Hakikisha CV yako inasomeka kiurahisi na inawasilisha mafanikio yako kwa uwazi.

Tumia maneno yanayoonyesha matendo

Maneno yanayo onyesha matendo yanaonyesha kwamba wewe ni mtu wa matendo, mchapa kazi. Maneno ya aina hii ni kama:

  • Kusimamia
  • Kupata
  • Kuchambua
  • Kusuluhisha
  • Kuboresha
  • Kufanya

Lengo la kutumia maneno kama haya ni kuonyesha uwezo na faida yako ndani ya mazingira ya kufanya kazi. Mwajiri anabidi aone mchango wako wa kikazi.

Anza na kazi yako ya sasa hivi au ya hivi karibuni alafu rudi nyuma. Hakikisha unafanya haya:

Ukiwa unaandika jina la kampuni uliyo fanya kazi, andika jina la kampuni kikamilifu. Pili, eleza kwa ufupi kampuni yao inahusika na nini. Tatu, weka muda uliyofanya kazi hapo (mwezi na mwaka). Baada ya hapo, orodhesha kazi na majukumu yako kwenye hiyo kampuni.

Tumia nambari na asilimia popote panapo faa

Kwa mfano, badala ya kuandika ‘nilichangia ongezeko la mauzo ya kampuni’ andika, ‘nilichangia ongezeko la mauzo ya kampuni kwa 25%’

Usidanganye

Hii ni tatizo kubwa sana Tanzania na ukidanganya, utagundulika tu na mwajiri akifanya utafiti wake juu yako. Ni sababu kubwa sana ya mtu kukosa ajira.

Maandalizi ya Mwisho

  1. Pitia kila kitu kwa mara ya mwisho

Makosa ya sarufi au ya kuandika maneno kadhaa yanaweza kusababisha ukose ajira kwa kuwa yanaonyesha kwamba hauko makini na kazi yako.

Dokezo la ziada: Chapisha CV yako alafu ipitie ikiwa kwenye karatasi. Hii huwa inasaidia kuona makosa yako.

  1. Rafiki apitie CV

Muombe rafiki yako apitie CV yako. Macho manne ni bora zaidi ya mawili!

Hatua ya kwanza kwenye kupata kazi unayotaka ni kutuma maombi. Tunatumaini kwamba vidokezo vilivyo elezwa humu vitakusaidia kuandaa CV bora kwa ajili ya mwajiri.

Sasa, kwa kuwa umeshajua jinsi ya kuandika CV safi, anza kutafuta kazi unayoitaka!

Bofya hapa kutafuta kazi unayoitaka leo!

 

Jinsi ya kuhakikisha wafanyakazi wako wanafuraha na kuongeza faida
Jinsi ya kufanya kazi na Bosi msumbufu