Naikumbuka siku moja niliyopigiwa simu na rafiki yangu kipenzi, tuliyekuwa tukitumiana nafasi za kazi kila tunapoona kwenye magazeti. Sauti yake ilisikika kama mtu aliyeshinda kesi ya kuwa mmiliki wa Benki Kuu ya Uswizi.

“Kupigika tupa kuleee… ni mwendo wa ki-corporate,” ni kati ya sentesi alizozitaja aliponieleza kuwa amepata kazi rasmi kwenye benki moja maarufu katikati ya jiji la Dar es Salaam. Kwa furaha alijikuta amevunja siri ya wengi, kwa kunitajia mshahara mnono anaopewa pamoja na ‘marupurupu’ lukuki yanayoambatana na mkopo wa gari. Tulishangilia kama vichaa wa muda, ‘woyooo… woyoo’ tukajua matatizo kwisha.

Kwa kupitia simu ileile, miezi mitatu baadaye, alinipigia nikiwa Mwanza, sauti yake ilikuwa ya chini kama mwenye mafua makali. Aliniambia kwa unyonge, anatamani kuachana na ile kazi na ameanza kuomba kazi benki nyingine! Hakuwa na sababu nyingine zaidi ya kumtupia lawama Bosi wake mwenye asili ya bara Asia. “Huyu Bosi kimeo sana, yaani ananipa stress (msongo wa mawazo), sina raha kila kitu anagomba tu,” alisema huku akiwa ndani ya gari lake la mkopo ambalo hakulijali tena kuwa linatokana na Bosi yuleyule anayemlalamikia.

Vilio hivi na stress za ofisini ni kawaida sana kwa waajiriwa wengi, lawama zikipelekwa kwa waajiri wao au wasimamizi wao wa kazi bila kujua kuwa wale ni binadamu ambao nao wana matatizo yao yanayowasukuma wakati mwingine kuwa wanavyokuwa. Au wana ndoto na malengo ambayo wanaona unakowapitisha hawatafika.

Hizi ni njia tano za kuweza kuishi kwa amani na Bosi anayekupa stress

  1. Weka mkakati wa kumsoma

Kabla hujaanza kuwaza jinsi ambavyo Bosi wako anakupasua kichwa mara kwa mara, anza kumsoma vizuri nini hasa anachotaka. Msikilize kwa umakini hata anapogomba na chambua lengo la mwisho analotaka kutoka kwako. Usiende na mdundo wa sauti zake za juu au kugomba, chagua kimkakati anachokitaka zaidi ya anachokisema.

  1. Kuwa mbele yake!

Baada ya kumsoma vizuri kimkakati, anza kuwa mbele ya hatua unazoamini anaweza kuzichukua anapokupa kazi yake. Fanya kazi zake kwa muda na jipunguzie muda wa mwisho (deadline) kutoka kwa ile aliyokupa ili usimkwaze.

Mfano: Mfanye asome barua pepe yako isemayo, ‘Samahani Bosi, ile kazi uliyonipa nimeiwasilisha tayari kwenye meza yako’, badala ya kusubiri aulize ‘kazi niliyokupa iko wapi?’.

Fahamu anachokitarajia kutoka kwako na fanya zaidi ya anachokitarajia.

  1. Tumia tabia ya ‘dada wa GPS’

Kama umewahi kutumia ‘Global Positioning System (GPS)’ au Google Map, kwenye simu yako ya kupapasa, kukuelekeza unapokwenda utafahamu uvumulivu wa hali ya juu wa msichana ambaye sauti yake unaisikia. Hata kama utakosea vipi uelekeo, hachoki kukuelekeza kwa ustaarabu. Hata unapokaidi anaposema pita kushoto, wewe ukapita kulia hachoki, atabadili na kukuelekeza tena.

Kuna wengi hulalamika kuwa Bosi haridhishwi na kazi zake hata anapojaribu kumridhisha. Cha msingi, fahamu kuwa ni Bosi wako, usijaribu hata siku moja kumuonesha kuchoka au kukasirishwa na anachokwambia. Msikilize, mshauri lakini maamuzi muachie yeye. Kuwa na tabia ya dada wa GPS.

  1. Jisimamie

Fahamu kuwa huwezi kumbadili Bosi wako, lakini wewe unaweza kufanyia kazi mwenendo wako na ukajibadili. Jiulize “ni nini chanzo cha matatizo kati yako na Bosi, na je, mimi ninaweza kufanya nini kubadili hali hiyo?”

Jiangalie wewe zaidi, usitumie hisia zako, tumia akili zaidi na tambua nafasi yako dhidi ya Bosi.

  1. Kuwa Msaada kwake

Kama Bosi wako anaonekana ana matatizo ya kutojali au kuwa na mambo mengi kiasi cha kushindwa kufuatilia kwa karibu mambo muhimu yanayohusu idara yako, kuwa msaada kwake. Mkumbushe kuhusu mwisho wa kazi (deadlines) na upendekeze suluhisho bila kuchoka.

Hapa uamuzi ni wako, kuendelea kuteseka na kunung’unika au kuchukua hatua tajwa hapo juu ili kuboresha mazingira yako ya kazi. Usikimbie!

  1. Fahamu wewe Sio Mkamilifu

Fahamu kuwa wewe sio mkamilifu, chukulia changamoto za kukusoa hata kama ni kwa sauti usiyoipenda kuwa ni fursa kwako kujifunza zaidi na kuwa bora. Anapokwambia kuwa kazi uliyompa haifai au hata kutumia neno ‘ni takataka’, usipaniki. Muulize kwa umakini na utulivu namna bora zaidi ya kuifanya kazi hiyo.

Kwa kujifunza kufanya kazi kwa namna anavyotaka iwe kutakufanya wewe kuwa bora zaidi sio tu kwa ajili yake lakini pia kwa siku za usoni.

  1. Jipumzishe

Unapomaliza kazi, rudi nyumbani na usichukue mahangaiko ya kazini na kuyahamishia nyumbani. Hakikisha kila unaporudi nyumbani inakuwa ni mapumziko haswa kutoka kazini. Acha kabisa… kabisa kumsimulia mkeo, mumewe ubaya wa Bosi wako kwani mtaanzisha mjadala usiokwisha kila siku mkimzungumzia alichofanya au alivyokuudhi.

  1. Ongea na Afisa Utumishi

Mtu pekee wa kumueleza matatizo yaliyopo kati yako  na Bosi wako ni Afisa Utumishi. Narudia tena, ‘kumueleza sio kumsemea’. Ongea naye, wao ni wataalam wanaweza kutumia njia bora zaidi za kuzungumza naye kama utaona kinachoendelea kati yenu ni kizito zaidi licha kufanya jitihada zote ulizoshauriwa hapo juu.

Kumbuka kukimbia tatizo hakujawahi kuwa suluhisho, hakuna sehemu bora ziaidi ya ulipo kwani ndiko kunakotengeneza njia ya yote yatakayofuata.

Chapa Kazi!

Ndugu wadai rambirambi za Masogange bongo movie waamua yao
Zitto amshauri Spika Ndugai