Mwenyekiti wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete ambaye leo anang’atuka katika madaraka ya uenyekiti wa chama hicho ameeleza namna ambavyo alimshawishi Rais John Magufuli kukubali kuwa mwenyekiti wa chama hicho kuanzia muda mfupi ujao.

Akizungumza katika mkutano mkuu maalum wa chama hicho kabla ya kumpitisha Dk. Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Dk. Kikwete amebeza na kuwapiga vijembe waliokuwa wakisema kuwa amekataa kujivua uenyekiti.

Alisema kuwa yeye ndiye aliyemshawishi Rais Magufuli kukubali kuchukua nafasi hiyo ingawa bado kikatiba angeweza kuendelea kwa miaka mingine miwili. Alisema kuwa Rais Magufuli alimkatalia awali na hivyo aliamua kumtuma mzee Phillip Mangula aliyefanikisha kumshawishi.

“Haikuwa rahisi kwa Dk. MagufuliJ kukubali kuwa mwenyekiti wa CCM lakini tulifanya kazi ya ziada kumshawishi akakubali,” alisema Kikwete.

Alisema kuwa aliona ni busara kuendelea kuheshimu maamuzi yaliyofanywa na watangulizi wao kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa Mwenyekiti wa chama hicho tawala.

“Wazee waliona mbali kuamua hivyo. Asiyesikia la mkuu guu huota tende. Na mimi sikutaka guu langu liote tende,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Kikwete amesema kuwa hadi leo anapong’atuka katika madaraka ya chama hicho, anakuwa amekitumikia chama kwa miaka 41. Alisema kuwa kutokana na namna alivyokitumikia chama kwake kustaafu ni jambo la kawaida na ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida anayeshirikiana na viongozi pale anapohitajika.

Wajumbe 2398 kati ya 2412 wamehudhuria mkutano huo ambao ni sawa na asilimia 99.4 na wanatarajia kupiga kura ya kumuidhinisha Dk. Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Kikwete awashtaki CCM kwa Magufuli, amtaka ashughulikie haya
Chid Benz afunguka kama amepewa shavu la kujiunga na WCB