Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema timu ya soka ya taifa, Taifa Stars ina mtihani mgumu mbele ya Algeria.

Taifa Stars inamenyana na Algeria, mwezi ujao katika hatua ya mwisho ya mchujo ya kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2016 Urusi.

Na akizungumza katika hafla ya kupongezwa kwake na Wanamicheo juzi ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Rais Kikwete alisema kwamba Algeria ni timu nzuri.

Alisema Algeria ndiyo timu ya Afrika iliyofanya vizuri zaidi ya zote kati ya zilizoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka jana Brazil, nyingine zikiwa ni Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon.

Kwa sababu hiyo, Rais Kikwete amesema huo ni mtihani mgumu kwa Taifa Stars, ingawa ameitakia kila la heri timu hiyo kuelekea mchezo huo.

Tanzania imeitoa Malawi katika hatua ya kwanza ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 nyumbani na Jumapili kufungwa 1-0 Blantyre.

Na baada ya matokeo hayo, Taifa Stars itamenyana na Algeria katika hatua ya mwisho ya mchujo, mechi ya kwanza ikichezwa Dar es Salaam Novemba 14 na marudiano Novemba 17 Algiers.

Rais Kikwete pia alilaani tabia ya makocha kufukuzwa baada ya timu kufungwa. “Huku kwetu timu ikifungwa, kocha anafukuzwa.

Sasa mnacheza na Algeria, ni timu bora Afrika, timu ambayo ilifanya vizuri zaidi ya zote kwenye Kombe la Dunia mwaka jana,”alisema.

Aidha, Rais Kikwete amesistiza kocha mzalendo Mkwasa, alipwe kama ambavyo walikuwa wanalipwa makocha wa kigeni. “Siyo kwa sababu Mluguru tu wa Morogoro basi, asilipwe vizuri,”alisema.

John Bocco Atuma Salamu Jangwani
Rais Kikwete Aonya Wanaobaki Vituoni Kulinda Kura, Mbowe Aja Na Yake