Mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans, watamenyana na JKU ya Zanzibar siku ya Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, katika mchezo wa kirafiki, ambao utakuwa wa kwanza tangu mabadiliko ya benchi la Ufundi mwezi uliopita.

Mwezi uliopita uongozi wa Young Africans ulileta Maofisa wapya wawili wa benchi la Ufundi, Kocha Mkuu George Lwandamina na Msaidizi, Noel Mwandila wote Wazambia.

Aliyekuwa Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm anakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wakati wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, Juma Pondamali kocha wa makipa, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli Jacob Onyango na Mtunza Vifaa, Mohammed Omar ‘Mpogolo’ wanaendelea kufanya kazi chini ya Wazambia.

Na baada ya mabadiliko hayo, Young Africans watacheza mchezo wa kwanza Jumamosi dhidi ya wakali wa Visiwani, JKU ambao utakuwa maalum kuiandaa timu kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Siku hiyo mashabiki wa Young Africans watapata fursa ya kumuona kwa mara ya kwanza kiungo Mzambia, Justine Zulu aliyesajiliwa mapema mwezi huu.

Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Desemba 17 na Young Africans itafungua dimba na JKT Ruvu Stars, iliyofanya mababadiliko ya benchi la Ufundi pia, ikimleta kocha Bakari Shime.

Mjema akutana na wachina, lengo ni kuiweka safi manispaa ya ilala
Aliyenusurika Ajali Ya Ndege Aanza Kutembea