Kitengo cha Afya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kimeweka udhibiti wa kujikinga na usambazaji wa magonjwa ambukizi ukiwemo ugonjwa wa Ebola.

Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka.

Afisa Afya Mfawidhi wa JNIA, Dkt. George Ndaki amesema kuwa wanatoa mafunzo kwa watumishi na wahusika wote wanaotumia kiwanja hicho katika kujikinga na magonjwa hayo.

“Sisi tumejiandaa vizuri na tumeshafanya jitihada zote tumeshatoa maelekezo, mafunzo na kamati mbalimbali za kiwanja zimejipanga kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza, ikiwemo sisi wenyewe kujikinga na kuwakinga na abiria wote wanaotoka katika nchi hatarishi,” amesema Dkt. Ndaki.

Aidha akizungumzia kuhusiana na utaratibu ambao Kiwanja kimeweka ili kuhakikisha abiria wenye maambukizi wanapokelewa kwa tahadhari wanapowasili na ndege zinazotoka nje ya nchi na zinazopakia abiria wanaosafiri kutoka katika nchi zinazoshirikiana na Kongo amesema kuwa abiria hutakiwa kusafisha mikono kwa dawa maalum mara waingiapo katika eneo la kuwasili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha amesema kuwa tayari JNIA wanazo taarifa za mlipuko wa ugonjwa huo na taratibu zote zimeshachukuliwa kwa kuwakagua abiria wanaotoka nje ya nchi.

Hata hivyo, Dkt. Ndaki amesema kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ambaye amebainika kuwa na ugonjwa wa Ebola kupitia JNIA.

 

Breaking: Pole Mh. Sugu kwa kufiwa na mama yako mzazi
Video: Rais Mstaafu Kikwete akwea Pipa kuelekea nchini Zimbabwe