Nahodha na Mashambuliaji wa Simba SC John Bocco amekiri mambo kuwa magumu msimu huu kwa klabu hiyo, baada ya kuambulia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC jana Jumatano (Mei 18).

Simba SC inayoshikilia Taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu minne mfululizo, ilicheza Uwanja wa ugenini Azam Complex-Chamazi jijini Dar es salaam, na kulazimisha sare hiyo, kufuatia bao lililofungwa na Bocco dakika chache baada ya Azam FC kutangulia kupitia kwa Rodgers Kola.

Bocco amesema mwanzoni mwa msimu huu walijiwekea lengo la kuendelea kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara, lakini hadi sasa mambo yamekua magumu kutokana na mwenendo wao kutoridhisha.

Hata hivyo Mshambuliaji huyo aliyemaliza kinara wa mabao msimu uliopita katika Ligi Kuu Tanzania Bara, amesema wataendelea kupambana hadi mwisho ili kuisaidia klabu ya Simba, ambayo inaendelea kushika nafasi ya pili kwenye Msimamo, ikiachwa kwa tofauti ya alama 10 na Young Africans iliyo kileleni.

“Kabla ya msimu huu kuanza tulijiwekea malengo ya kuendelea kutata taji letu kwa mara ya tano mfululizo, lakini mambo yamekua tofauti hadi sasa, lakini bado tutaendelea kupambana kwa sababu msimu haujakwisha,”

“Matarajio kwenye Ligi Kuu kwa hakika yameshafifia, lakini kwenye Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ tunaendelea kufukuzia ubingwa wetu ili tuweze kuutetea, kwa hiyo huku tutapambana zaidi ili kuangalia tutapata nini kwa msimu huu.”

“Tunaamini tutamaliza msimu vizuri, huku kwenye Ligi hatukuwa Bora, lakini kwenye Kombe la Shirikisho tunatarajia makubwa zaidi kwa sababu kuna nafasi ya kufanya jambo na tukamaliza vizuri, tena tukiwa Bora.” amesema John Bocco

Simba SC itacheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Young Africans Jumamosi (Mei 28), Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku Azam FC ikitarajia kukutana na Coastal Union Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jumapili (Mei 29).

Wazazi wa Martha Karua wasimulia ukuaji wake, Ni Hodari, Mahiri na mwenye Maamuzi
28 wafariki wakigombea mifugo