KATIBU Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Johnson Chinyong’ole amesema aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentine Mokiwa anakabiliwa na mashitaka ya jinai kwa kuingia mikataba mibovu na matumizi mabaya ya fedha za kanisa makosa yanayoangukia kuvunja sheria za nchi.
“Hatujakurupuka kuchukua hatua, ushahidi wote tumeshauwasilisha kwa vyombo vinavyohusika serikalini, sisi tumetimiza wajibu wetu, hivyo tunaviachia vyombo vinavyohusika kufanya kazi yake katika eneo hilo la ubadhirifu wa fedha,” amesema Chinyong’ole.
Amesema kuwa wakati wanaenda kutangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa juzi kanisa la Ilala, walienda kutoa taarifa kwa msajili wa vyama ambaye ndiye anayesajili makanisa, lakini pia wameshatoa taarifa katika ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
Katibu Mkuu huyo amesema ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi ya askofu huyo yenye kurasaa 173 imewasilishwa pia serikalini ili vyombo vinavyohusika kufuatilia tuhuma hizo viweze kujiridhisha wakati vinapoenda kuchukua hatua
Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauri nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya ufujaji wa mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi ya kanisa hilo nchini.
Hata hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa, mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Salaam ambayo ndio yenye uamuzi wa kumfuta kazi na si askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania

UVCCM Yatoa onyo kwa Lowassa na Maalim Seif
Ni Patashika Nguo Kuraruka, Nani Kukosa Usingizi Leo?