Viongo Jonas Mkude na Clatous Chotta Chama wamekosa mazoezi ya mwisho ya kikosi cha Simba SC kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa 24 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam.

Simba SC imefanya mazoezi yake ya mwisho katika Uwanja wa Uhuru leo Jumanne (Mei 17) asubuhi, chini ya maafisa wote wa Benchi la Ufundi, ambalo linaongozwa na Kocha kutoka nchini Hispania Franco Pablo Martin.

Miamba hiyo itakutana kesho Jumatano (Mei 18) kuanzia mishale ya saa moja usiku, huku kila upande ukihitaji alama tatu muhimu ili kujiongeza kwenye mapambano ya Ligi Kuu inayoelekea ukingoni.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amethibitisha kukosekana kwa wachezjai hao katika mazoezi ya mwisho ya kikosi cha Simba SC, kutokana na hali zao kuendelea kuwa mtihani kutokana na majereha yanayowakabili.

“Ni kweli Chama na Mkude wamekosa mazoezi ya Simba SC kuelekea mchezo wetu na Azam FC kesho Jumatano, kutokana na hali zao kuendelea kuwa mtihani, hivyo tutawakosa kwenye mchezo huo, ambao tumejipanga kwenda kupambana na kupata matokeo.”

Katika hatua nyingine Ahmed Ally amewataka mashabiki wa Simba SC kufika kwa wingi kwenye Uwanja wa Azam Complex, kwa ajili ya kuipa nguvu timu yao kama walivyofanya kwenye michezo mingine waliocheza katika uwanja wa nyumbani na viwanja vya ugenini msimu huu.

“Simba ina mashabiki wake, tunahitaji wafike Uwanja wa Chamazi kuja kuipa nguvu timu yao, tunaamini kuja kwao kwa wingi kutaongeza kitu katika harakati za timu yetu kusaka ushindi ambao utakua na manufaa makubwa kwenye mbio za kuelekea mwishoni mwa msimu.” amesema Ahmed Ally

Simba SC inakwenda ugenini Azam Complex ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 49, huku mwenyeji wake Azam FC akishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 32.

Nyuma ya 'Dakika 23 za CINEMA' ya Maua Sama amesimama FA
Tukio la Afrika Kusini, Simba SC yaomba radhi