Nahodha na beki wa klabu ya Southampton Jose Fonte amepinga mpango wa kuwa kwenye orodha ya meneja wa Man Utd Jose Mourinho, kwa kusema hafikirii kuondoka St Mary’s Stadium.

Fonte ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kilichotwaa ubingwa wa Euro 2016, amekua anaripotiwa kuwa mbioni kusajiliwa na Man Utd kwa shinikizo la Jose Mourinho itakapofika mwezi Januari mwaka 2017.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 32, amesema pamoja na uwepo wa taarifa hizo, hana budi kuheshimu mkataba wake wa kuitumikia The Saints na hadhani kama ataondoka klabuni hapo kwa sasa.

“Nimekua ninaona taarifa zinazonihusu kupitia mitandao ya kijamii na kwenye baadhi ya magazeti, lakini niufahamishe umma kwamba, sina mpango wa kuondoka Southampton kwa sasa,” Alisema Fonte

“Ninajivunia kuwa mchezaji wa Southampton, na ninaamini uwepo wangu hapa ndio chachu ya kuendelea kusaka mafanikio kwa kusaidiana na wenzangu.

“La msingi kwangu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika ligi ya nchini England na michuano ya kimataifa, lingine ni kuisaidia timu yangu ya taifa ili ifanikiwe kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia, hayo mengine ya kuhamia Man Utd sina mpango nayo.”

Kwa sasa Fonte yupo kwenye kambi ya timu ya taifa ya Ureno ambayo inajiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, ambapo mwishoni mwa juma hili itacheza dhidi ya Latvia mjini Algarve.

Breaking News: Moto mkubwa wazuka Kiwandani (Video)
Mamadou Sakho Kurudi Ufaransa?