Meneja wa klabu ya Tottenham Hospurs Jose Mourinho, amesema hana njia nyingine zaidi ya kuhakikisha anakamilisha mpango wa kumsainisha mkataba mpya kiungo mkabaji kutoka nchini England, Eric Jeremy Edgar Dier.

Mourinho ameahidi kukamilisha mpango huo, kufuatia mkataba wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu ujao, na bado hajaanza mazungumzo na uongozi wa Spurs.

Mourinho amesema amekua akiushawishi uongozi kufanikisha mpango wa kuanza mazungumzo na kiungo huyo, na tayari ameanza kuona dalili za jambo hilo kufanyika siku za karibuni.

Amesema uongozi umemuhakikisha kukutana na Dier ili kuanza mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya, hivyo ana imani mambo yatakwenda vizuri.

“Bosi wangu ameniambia anahitaji kumuona Dier akisaini mkataba mpya, nimeongea na mchezaji ameniambia anafuraha kuendelea kuwa hapa, hakuna haja ya kumuacha aende kwingineko” alisema Mourinho.

“Nadhani kutakuwa na maelewano mazuri kwa sababu tunaelekea kwenye mwongozo mzuri”.

Dier amecheza michezo miwili kama mlinzi wa kati nafasi ambayo anaipendelea zaidi tangu kuanza kwa ligi katika awamu ya pili, baada ya kusimama kwa takribani miezi mitatu kutokana na janga la virusi vya Corona.

Meneja wa zamani wa Tottenham Mauricio Pochettino alikuwa anapendelea kumtumia mchezaji huyo kama kiungo mkabaji, lakini tangu alipoajiriwa Mourinho, Dier muda mwingine amekuwa akimtumia kama beki wa kati.

Dier, alijiunga na Spurs kwa dau la pauni milioni 4 akitokea Sporting Lisbon mwaka 2014, na tayari ameshaifungia klabu hiyo mabao 10 katika michezo 171.

Hali ya Kapombe inaridhisha
Uchaguzi 2020: Watanzania waombwa kulinda amani