Meneja wa Man utd Jose Mourinho amemtaka Paul Pogba kuhamishia uwezo na ujasiri aliouonyesha wakati wa fainali za kombe la dunia zilizomalizika nchini Urusi Julai 15, kwenye kikosi cha Man Utd pindi atakaporejea na kujiunga na wenzake kwa ajili ya msimu mpya wa ligi.

Akiwa nchini Marekani kwa ajili ya ziara ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ya England, meneja huyo kutoka nchini Ureno, amesema kwa hakika Pogba alicheza vizuri wakati wote wa fainali za kombe la dunia, na kufanikisha lengo la nchi yake kutwaa ubingwa wa fainali hizo.

Mourinho anaamini kiungo huyo mwenye asili ya bala la Afrika, atakua na uwezo kama huo, pindi atakaporejea klabuni hapo, ili kufanikisha malengo ya kutwaa ubingwa wa England kwa msimu ujao.

‘Nimeshazungumza na Pogba, nimemwambia uwezo na ujasiri aliouonyesha akiwa Urusi ninauhitaji ndani ya kikosi changu kwa msimu ujao,’ Alisema Mourinho alipohojiwa na kituo cha televisheni cha ESPN.

‘Naamini fainali za kombe la dunia zimeonyesha namna mchezaji huyu alivyo na uwezo wa kucheza soka la hali ya juu, siamini kama itashindikana atakapokua nasi kwa msimu ujao.”

‘Tunahitaji kucheza kitimu kama ilivyokua kwa Uafaransa, na ukiangalia mtu muhimu katika timu ile alikua Pogba, hivyo ninataka hata akirejea hapa Man utd awe mtu muhimu kwa kutafuta namna ya kuiwezesha timu kushinda.”

Pogba anatarajiwa kurejea Old Trafford mwanzoni mwa mwezi ujao, tayari kwa kujiunga na wachezaji wenzake wa Man Utd, kwa ajili ya msimu mpya wa ligi utakaoanza Agusti 11.

Kiungo huyo alipewa likizo ya mapumziko, baada ya kukamilisha kazi ya kulitumikia taifa lake kwenye fainali za kombe la dunia zilizomalizika Julai 15, na kushuhudia Ufaransa wakiibuka mabingwa kwa mara ya pili baada ya miaka 20.

Rais Magufuli amteua Mkapa kumuwakilisha Msumbiji
Lugola amsweka ndani askari polisi kwa uzembe

Comments

comments