Chama cha soka nchini England (FA), kimemfungulia mashtaka meneja wa Man Utd Jose Mourinho, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha wakati wa mchezo wa ligi wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya West Ham utd, uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.

Mourinho alipandwa na hasira na kufikia hatua ya kupiga teke chupa ya maji iliyokua pembeni yake, baada ya kukasirishwa na hatua ya kiungo wake Paul Pogba kuonyeshwa kadi ya njano.

Kitendo hicho kilimlazimu mwamuzi Jonathan Moss kumuondoa katika benchi la ufundi la Man Utd, na kumuamuru akae jukwaani.

“Ni tabia iliyokua kinyume na kanuni za ligi ya England… Ni utovu wa nidhamu,” ilieleza taarifa iliyotolewa na FA. “Ana muda wa kujitetea hadi Disemba mosi saa kumi na mbili jioni.”

Hata hivyo Mourinho hakuzungumza na vyombo vya habari mara baada ya mchezo dhidi ya West Ham Utd kumalizika katika uwanja wa Old Trafford, na badala yake alimtuma msaidizi wake Rui Faria.

Faria alisema: “Nafikiri kila mmoja ameona ni vipi Mourinho alivyochanganyikiwa baada ya kitendo cha kadi ya njano kumkabili Pogba.

“Huenda ikawa ngumu kwangu kuelezea namna alivyochanganyikia hadi kufikiahatua ya kupiga teke chupa iliyokua karibu yake, lakini ninataka mfahamu kwamba hakupendezwa na maamuzi yaliyokua yanaelekezwa kwetu.”

Mourinho anaamini mwamuzi alimuonea Pogba kwa kumuonyesha kadi ya njano, kwa kisingizio cha kumchezea rafu kiungo wa West Ham Utd Mark Noble, ambaye anadaiwa alijiangusha kwa makusudi.

Mourinho, ameshaadhibiwa kwa kufungiwa mchezo mmoja na chama cha soka nchini England (FA) mwezi uliopita, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha walipopambana na Burnley, ambao walilazimisha sare ya bila kufungana katika uwanja wa Old Trafford.

Philippe Coutinho Kusubiri Hadi 2017
Ali Kiba amkejeli Diamond kuhusu ‘Pete ya Kijani’