Wachezaji wa klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shaaban Iddy Chilunda na Joseph Kimwaga waliokuwa majeruhi, huenda wakarejea dimbani Januari Mosi mwakani wakati timu hiyo ikishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.

Mbali na kufanya programu ya mazoezi ya gym, mshambuliaji Iddy Chilunda ameruhusiwa kuanza mazoezi madogo madogo ya kucheza na mpira na kukimbia mwanzoni mwa wiki hii huku Kimwaga akiendelea na mazoezi ya gym aliyoanza mwezi mmoja uliopita.

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa amesema kuwa wachezaji hao wapo kwenye kipindi cha mwisho cha tiba yao cha kuwarejesha katika hali yao ya kawaida huku akidokeza Idd ataendelea na programu hiyo na anatarajiwa kurejea dimbani kuanzia Januari Mosi.

“Kimwaga kidogo kumetokea matatizo kidogo katika ukunjaji wa goti lake baada ya operesheni kwa hiyo sasa hivi bado anafanya mazoezi ya kukunja goti na pindi atakapokuwa ameweza kukunja goti vizuri naye ataruhusiwa kuanza kucheza mpira kidogo kidogo na kukimbia naye pia tutamtarajia itakapofika Januari Mosi atarudi tena kiwanjani kwenye ushindani,” alisema.

Iddy anasumbuliwa na majeraha ya nyonga yake ya mguu wa kulia huku Kimwaga akisumbuliwa na goti la mguu wa kushoto kwa pamoja walifanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini na tokea waanze mazoezi ya gym wamekuwa chini ya uangalizi wa daktari wa Azam FC na wataalamu wa Kliniki ya London Health Centre, iliyopo eneo la Macho, Msasani jijini Dar es Salaam wanakofanya mazoezi ya gym.

Yondani, Tshishimbi, Tambwe kuwavaa maafande wa Prisons
LIVE: Rais Magufuli akihutubia katika uzinduzi wa hospitali ya taaluma na tiba, Mloganzila