Mbunge wa Geita Vijijini na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma, amekana kupokea kiasi chochote cha fedha kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ili amuunge mkono.

Msukuma akimnadi Lowassa

Msukuma akimnadi Lowassa

Msukuma alikuwa mtu wa karibu wa Lowassa aliyempigania katika kinyang’anyiro cha kusaka nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM akitumia helicopter (chopa) kumnadi Lowassa, kabla hajahamia Chadema.

Akizungumza leo katika kipindi cha Tuongee Asubuhi cha Star TV, Msukuma alisema kuwa hakupewa pesa na Lowassa kufanya kazi hiyo, bali alifanya kwa moyo wake akiwa katika harakati za kutafuta kura za CCM.

“Mimi sijapewa hata shilingi moja na Lowassa,” alisema. “Na mimi nataka nimwambie Waitara (Mbunge wa Ukonda) ajaribu kukaa na Rais wake huyo aliyeshindwa [Lowassa], amuulize alinipa shilingi ngapi? Ninaweza kurudisha. Lakini nimwambie mimi nilienda kutafuta kura za CCM,” aliongeza.

Alisema kuwa yeye alimfanyia kampeni Lowassa wakati huo kama askari aliyetumwa kwa adui ili ajifunze mbinu zake na baadae azitumie kupambana naye.

Aidha, alisema kuwa yeye ndiye aliyemfundisha Lowassa jinsi ya kuharibu ‘itifaki’ ya CCM, na kwamba anamjua udhaifu wake zaidi ya upinzani wanavyomjua.

“Na katika watu walioharibu kura za Lowassa, mimi ndiye niliyeharibu, na katika watu waliomfundisha Lowassa kuharibu itifaki ya CCM, mimi ndiye nilikuwa front (mbele) kwenye helcopiter yake natua kila sehemu,” alisema.

Lowassa alihamia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa baada ya Kamati Kuu ya CCM kulikata jina lake.

 

Video: Itazame Chapaa ya GentrIez ft. Belle 9 na Young Dee
Rais ataja majina ya wauza ‘Unga’, wamo majaji, wabunge