Kocha mpya wa Simba, Joseph Omog anatarajia kuanza kazi leo huku akitaka wachezaji wote waliosajiliwa Simba kuwepo katika mazoezi ya timu hiyo bila kukosa.

Mbali na wachezaji waliosajiliwa, Omog amewataka pia wachezaji ambao bado hawajamwaga wino, lakini wanatarajiwa kusajiliwa na timu hiyo. Omog raia wa Cameroon, ameuambia uongozi angetaka kumuona kila mchezaji wa Simba akiwa mazoezini.

Mara nyingi timu za Tanzania zimekuwa na mahudhurio hafifu ya wachezaji siku ya kwanza ya mazoezi, huku wale wanaochelewa kuripoti wamekuwa wakiibuka na visingizio lukuki.

Naye msemaji wa timu hiyo, Haji Manara alisema kocha huyo leo atakabidhiwa rasmi timu hiyo kwa ajili ya kuanza kuinoa tayari kwa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.

Manara alisema kocha huyo mpya baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wiki iliyopita na kutambulishwa kwa vyombo vya habari, leo atakutana rasmi na uongozi kwa ajili ya kukabidhiwa timu.

“Tutakutana na kocha na kuweka mikakati yetu ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.Baada ya kukutana naye tutawatumia taarifa ya mikakati yetu ya kambi na suala zima la usajili,” alisema.

Omog ambaye aliwahi kuifundisha Azam FC na kuipa taji la Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa mwaka 2013-14, atakabidhiwa pia wachezaji wapya, ambao tayari wamesajiliwa kwa ajili ya kuungana na wale wa zamani kusaidia timu hiyo kufanya vyema.

Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa hivi karibuni ni Mohamed Ibrahim, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Emmanuel Simwanza, Ame Ally, Shiza Kichuya na Jamal Mnyate. Pia, inatarajia kusajili wengine akiwemo Mrundi Laudit Mavugo na Muivory Coast Goue Blagnon aliyetarajiwa kutua jana usiku akiwa na kipa wa Simba Vicent Angban.

Wachezaji wengine wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi hicho ni Jonas Mkude, Peter Manyika, Angban, Denis Deonis, Salum Kimenya, Mohamed Hussein na Abdi Banda. Pia, wapo Awadh Juma, Said Ndemla, Daniel Lyanga, Hassan Kabunda, Haji Ugando, Mbaraka Yusuf, Justice Majabvi na Musa Ndusha.

Ujio wa Omog unatarajiwa kuleta matumaini mapya ndani ya kikosi hicho na mashabiki ambao wana uchu wa kupata taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara na michuano ya kimataifa. Akizungumza wakati wa kutambulishwa kwa waandishi wa habari, Omog alisema kuwa amekuja Simba ili kuondoa ukata wa mataji ulioikabili timu hiyo kwa muda mrefu sasa.

Makocha Wa Hispania Kumchambua Mmoja Mmoja Azam FC
Arsenal, Chelsea Zamuwania Romelu Lukaku