Katika kuhakikisha Wekundu wa Msimbazi hawarudii tena makosa ya kusajili wachezaji ‘vilaza’, Kocha Mkuu Joseph Omog amewatema wachezaji watano, kati yao wanne ni wa kigeni baada ya kutoridhika na viwango vyao.

Kikosi cha Simba kiko mjini Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na Kocha Omog – raia wa Cameroon, amekuwa makini kuchagua wachezaji wenye viwango vya daraja la kwanza kwa mahitaji ya ligi nyumbani na mashindano ya kimataifa.

Meneja wa Simba, Abbas Ally alisema jana kuwa, Omog hakuridhika na viwango vya wachezaji hao, hivyo hakuwa na namna zaidi ya kuwatema.

Waliofungashiwa virago ni pamoja na mshambuliaji wa FC Lupopo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Masoud Cedrick Masanga, kiungo wa klabu hiyo Sanga Bahende na straika wa zamani wa timu ya Panthere, Mcameroon Ndjack Anong Guy Serge.

Mchezaji mwingine wa kigeni aliyeshindwa kutembea kwenye mstari wa viwango vya ubora vya Omog ni kiungo kutoka Cameroon Derick. Mzalendo pekee aliyetemwa ni beki Khalfan Twenye kutoka African Sports ya jijini Tanga.

Hata hivyo, Ally alisema kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa kigeni wameonyesha viwango vizuri na huenda wakapewa karatasi kumwaga wino.

Nyota hao ni pamoja na mshambuliaji kutoka Ivory Coast Frederic Blagnon, Method Mwanjala (Zimbabwe), beki Janvier Bokungu na mshambuliaji Mussa Ndusha wa DRC.

Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele muda mchache uliopita amezungumza na Dar24.com na kusema kuwa bado mchakato wa kusaka wachezaji wa kigeni unaendelea kwa lengo kutimiza mahitaji ya benchi la ufundi.

Wachezaji wapya waliotua Msimbazi kutoka Mtibwa Sugar ni viungo Muzamil Yassin, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim na Shizza Kichuya.

Wengine ni Moses Chibandu, Said Mussa, Kelvin Falu, Vincent Costa, wakati wa zamani walioko kambini ni nahodha Mussa Hassan ‘Mgosi’ Juuko Murshid, Vincent Angban, Awadh Juma, Said Ndemla, Peter Mwalyanzi, Peter Manyika, Dennis Richard, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hijja Ugando, Novatus Lufunga, Mwinyi Kazimoto, Danny Lyanga na Ibrahim Ajib.

Aliongeza kuwa timu hiyo inatarajia kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu mjini Morogoro kabla ya kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya Tamasha la Siku ya Simba Agosti 8 kwenye Uwanja wa Taifa.

Audio: Waziri Mahiga azungumzia maamuzi ya Afrika kujitoa au kubaki ICC
Tusikubali Kuingia Kwenye Uchaguzi Mkuu Bila Katiba Mpya - Mngeja