Hatimaye Anthony Joshua amekata mzizi wa fitna kwa kumpiga mpinzani wake, Joseph Parker na kushinda mikanda minne ya ubingwa wa dunia wa masumbwi wa uzito wa juu ya WBA, IBF, IBO na WBO, katika pambano lililofanyika usiku wa kuamkia leo nchini Uingereza.

Kwa mara ya kwanza Joshua amepigana raundi zote 12 na kushinda kwa pointi 118-110, 118-110, 119-109. Ushindi ambao unaonesha bondia huyo wa Uingereza mwenye asili ya Nigeria aliteka zaidi pambano dhidi ya bondia huyo wa New Zealand.

Hata hivyo, wachambuzi wa mchezo huo wameonesha kutoridhishwa na jinsi mwamuzi alivyousimamia kwani hakuwa anawapa nafasi wawili hao kupambana zaidi akiwaachanisha mara kwa mara na kuingilia wakati ambapo vita inataka kuiva.

Wachambuzi wa mtandao wa Telegraph wa Uingereza wamedai kuwa umati uliohudhuria haukuona ‘vita’ waliyokuwa wakiitegemea na badala yake waliona mchezo uliogubikwa na umbali zaidi.

Baada ya ushindi huo, Joshua alinyoosha ngumi yake kwa mbabe ambaye hajawahi kupigwa, Deontay Wilder. Pambano la wawili hao litamfanya mshindi kufikia kiwango cha juu zaidi ya ubingwa wa masumbwi cha ‘undisputed champion’.

“Parker ni mpiganaji kijana na mzuri, nina uhakika nitapigana naye tena, lakini ngoja kwanza tumlete Deontay Wilder hapa ili tumpate ‘undisputed champion’ wa dunia.

Kwa upande wa Parker, hakuelekeza lawama zake kwa mwamuzi kama wengi walivyodhani.

“Najisikia vizuri. Natakiwa kufanya mazoezi zaidi kwa mambo mengi. Alikuwa mkubwa zaidi na bora zaidi leo, lakini nitarudi,” alisema Parker.

Pambano hilo limeweka doa kwenye rekodi ya Parker ya kutopigwa huku likimuongezea Joshua pambano moja la ushindi na doa moja la kutopiga KO (21-0-K20).

Profesa Kitila ajibu waraka wa maaskofu KKKT
Bavicha: Hakuna mwenye uwezo wa kuifuta Chadema

Comments

comments