Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari ameipongeza Serikali na kuahidi kushirikiana nayo bega kwa bega ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu kufuatia jitihada kubwa zianazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo mbalimbali nchini wakiwemo wa jimbo lake.

Nassari amesema hayo Desemba 18, 2016 mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 ya kikazi mkoani Arusha.

Amesema ameridhishwa na hatua mbali mbali za Serikali ikiwemo za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinazochukuliwa na Serikali.

Nassari amesema ziara ya Waziri Mkuu mkoani Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa yalitokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.”Kama kuna kiongozi ambaye hawezi kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu, atakuwa na matatizo.

Ameongeza kuwa kitendo cha Waziri Mkuu kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi ni ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wananchi wa kawaida.

Hivyo amempongeza Waziri Mkuu kwa kuamua kuitafutia ufumbuzi changamoto ya ardhi wilayani Arumeru jambo ambalo litawawezesha wananchi kupata ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kimaendeleo zikiwemo za  kilimo na ufugaji.

Kwa upande wake waziri Mkuu, Kassim Majaliwa asema kuwa Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki.

“Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” – Waziri Mkuu.

Amesema Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza..

 

Ridhiwani aomba waajiri kutoa nafasi kwa vijana, akemea dhana potofu...
Majaliwa aagiza kaburi la Faru John Lifukuliwe