Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Kagera kuijengea nyumba ya hadhi familia ya Leopord Mujungi aliyekuwa mkurugenzi wa barabara nchini na ambaye alisimamia Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha rami kutoka Dar es salaam hadi Mpaka wa Mtukula wilayani Misenyi mkoani Kagera ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa kulitumikia taifa.

Rais Magufuli amesema hayo mara baada ya kufika nyumbani kwa marehemu Mujungi aliyefariki kwa kujipiga risasi miaka kadhaa iliyopita na kuagiza familia hiyo ijengewe nyumba ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa kulitumikia taifa.

”Natambua mchango mkubwa wa mzee Mjungi alikuwa mkweli na alikuwa mwaminifu, mnaweza kuona mtu aliyekuwa mkurugenzi wa barabara zote hata nyumba yake ni ya kawaida, nakuagiza meneja wa Tanrods wasiliana na wizara nyumba ijengwe hapa hata kama ni shilingi milioni 50-100 ijengwe hapa” Ameagiza Rais Magufuli.

Akiwa njiani, Rais Magufuli amezungumza na wananchi katika eneo la Kyaka wilayani Missenyi, Kemondo wilayani Bukoba na Muleba ambapo akiwa wilayani Muleba amemuagiza pia waziri wa Nishati Dkt. Medadi Kaleman kwenda mkoani Kagera kutatua changamoto ya umeme, kufuatia kuwepo kwa wananchi ambao wamelipia umeme wa Rea awamu ya pili na hawajaunganishiwa umeme.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kagera ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mfumo mzuri wa ununuzi wa zao la Kahawa ya wananchi kwa kuwaharakishia malipo pamoja na ujenzi wa chuo cha Veta kitakachojengwa katika wilaya ya Bukoba, ambapo Ujenzi wa chuo hicho utagharimu jumla ya  shilingi bilioni 22.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 12, 2019
TANTRADE kuendelea kuimarisha mitandao ya Wafanyabiashara