Rais John Magufuli amewaagiza watendaji katika mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri utakaowawezesha wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga kufanya shughuli zao ndani ya stendi mpya ya Msamvu.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua rasmi stendi hiyo ya kisasa, ambapo amesitiza mtu wa aina yoyote asibaguliwe bali wafanyabiashara hao wadogo wapewe vitambulisho.

“Nimekuja kufungua stendi lakini sio kufungua stendi ya ubaguzi. Nimechaguliwa na Watanzania wote. Niwaombe tu mtengeneze mkakati mpya kuwawezesha wamachinga kuruhusiwa kuingia humu na wapewe vitambulisho,” alisema Rais Magufuli.

“Mnawanyima nafasi watu wa hapa maana hawatauza mihogo, machungwa na bidhaa zao kwa wasafiri wanaopita hapa,” aliongeza na kusisitiza kuwa fedha zisizojali maskini ni fedha haramu.

Dkt. Magufuli pia aliagiza hatua hiyo kufanyika kwa nchi nzima, akimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jaffo kuhakikisha kuwa kila stendi inakuwa na utaratibu utakaowawezesha machinga, mama ntilie na wengine kufanya biashara ndani ya stendi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameutaka uongozi wa mkoa huo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo mapato ya stendi hiyo, kwani taarifa alizopewa zinakinzana na mapato yaliyotajwa.

 

Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Mei 7, 2018
Waziri apigwa risasi kwenye mkutano wa kampeni