Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameagiza ofisi zote za Serikali kuhakikisha zinatumia huduma za TTCL katika kufanya mawasiliano.

Ametoa agizo hilo jana kwenye hafla ya kupokea gawio la pili kutoka katika taasisi hiyo ambayo tangu ilipoanzishwa imeonesha kupiga hatua ya faida kuanzia Mwaka wa Fedha uliopita.

Alionesha kushangazwa na kutotajwa kwa ofisi yake pamoja na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika orodha ya ofisi za umma zinazotumia huduma za TTL.

“Alipokuwa akitaja taasisi mbalimbali zilizojiunga kutumia TTCL, nilisikitika sana kusikia hata ofisi yangu ya Rais haikutajwa. Na nimesikitika pia hata chama changu cha Mapinduzi hakikutajwa,” alisema Rais Magufuli.

“Kwahiyo inaonekana hawa wapinga-wapinga hawa hata kwenye ofisi yangu wapo. Sasa kama wananisikia, kama wako hapa na huwa wamezoea kunisindikiza, nataka kipindi cha mwezi mmoja tuanze kutumia simu za TTCL,” aliongeza.

Aidha, alizitaka Wizara zote na ofisi za Serikali kuhakikisha zinajiunga mara moja na huduma za TTCL, kama majeshi mbalimbali yalivyofanya.

Hata hivyo, Rais Magufuli alifafanua kuwa hajawakataza watumishi wa umma kuwa na laini za mitandao mingine, lakini kwa wale ambao wanalipiwa na Serikali kutumia huduma za simu ni vyema wakawekewa sharti la kulipiwa kupitia laini za TTCL.

Alisema yeye binafsi anatumia line ya TTCL kufanya mawasiliano yake na analipa gharama zake mwenyewe, hivyo anawahamasisha watumishi wengine kuwa wazalendo na kuliunga mkono shirika hilo lililoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Makamba aonya virungu, upekuaji kudhibiti mifuko ya plastiki
Zitto afunguka unyanyasaji kuhusu uraia mipakani, Serikali yampa heko

Comments

comments