Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa waasisi wa Taifa na mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea alfajiri ya leo katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema kuwa taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya serikali.

“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu,”amesema Rais Dkt. Magufuli

Aidha, kufuatia msiba huo  Rais Dkt. Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo, na amewaomba kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Hata hivyo, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitalini ya Muhimbili baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam mnamo Disemba 22, mwaka 2017.

Ujumbe wa mwisho wa Zari kabla ya kum-unfollow Diamond
Mpina akamata meli Mtwara, aipiga faini ya mamilioni