Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemteua Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), akichukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene ambaye amekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Simbachawene amechukua nafasi hiyo baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Kangi Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara.

Rais Magufuli alimuondoa Lugola kwenye nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani akieleza kuwa wizara hiyo imehusika kusaini ‘mkataba wa hovyo’, na bila kufuata taratibu na sheria za nchi.

Alieleza kuwa Wizara hiyo ilisaini mkataba kati ya Jeshi la Uokoaji na Zima Moto na Kampuni Moja ya Romania, wenye thamani ya zaidi ya Sh. Trilioni 1 za Tanzania kama mkopo, huku wakifahamu kuwa Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo yenye dhamana ya kukopa kwa niaba ya Serikali.

Aidha, Rais amesema kuwa kutokana na sakata hilo, Kamishna wa Jeshi la Zimamoto, Thobias Andengenye pia hawezi kusalimika kwani alihusika katika kusaini mkataba huo bila kufuata taratibu na sheria za nchi.

Rais Magufuli amempongeza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kwa kuchukua hatua na kuomba kujiuzulu. Amesema anampenda na anamheshimu lakini hana budi kukubaliana na barua yake ya kujiuzulu.

Live: Rais Magufuli katika kikao na viongozi wa CCM
Polisi wakana kumkamata mwanafunzi wa UDOM