Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli amesema kuwa changamoto ambazo hazitapata ufumbuzi katika Serikali anayoiongoza, zinaweza zisitatuliwe na viongozi wengine wajao.

Ameyasema hayo leo katika hafla ya makabidhiano ya mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS), iliyofanyika kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano (TCRA), jijini Dar es Salaam.

“Kama kuna changamoto ambazo hazitatatuliwa awamu hii basi hazitatatuliwa maishani, kwa sababu sidhani kama hata anayekuja ataweza kuzitatua,” alisema Rais Magufuli na kuongeza, “Katika kushughulikia changamoto, yako magumu mengi sana.”

Amesema wapo watu wasio na nia njema ambao aliwafananisha na watu wabaya walio gizani ambao kwa hali ya kawaida huwezi kufahamu silaha walizonazo.

Hivyo, Rais Magufuli amewataka viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla kuliombea taifa kwani lipo katika vita ya uchumi ambayo sio vita rahisi.

Aidha, aliwapongeza viongozi wa TCRA kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwataka kusimama imara kwani anafahamu kuna changamoto nyingi wanazozipitia ikiwa ni pamoja na kupigwa vita.

Mfumo huo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu utakaokuwa chini ya TCRA, pamoja na mambo mengine, utahakiki mapato yote ya watoa huduma za mawasiliano na kubaini simu za ulaghai.

“Mfumo huu unapunguza urasimu na mfumo wa rushwa katika nchi yetu hivyo ni vyema kuitumia vizuri sekta hii ili ituletee maendeleo na si kutuletea madhara katika jamii ikiwemo mmomonyoko wa maadili,” alisema Rais Magufuli.

 

Mwanamke mgonjwa wa macho apewa dawa za nguvu za kiume, zamjeruhi
Ripoti: wanawake walalama ukata wa wanaume waoaji

Comments

comments