Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wanasiasa watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2020 kuzingatia sheria na kuepuka lugha za matusi.

Ameyasema hayo leo, Juni 16, 2020 alipokuwa akitoa hotuba yake ya kuvunja Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Magufuli amesema kuwa wanasiasa wanapaswa kushindanisha hoja na Ilani za Uchaguzi.

Mkuu wa Nchi ameongeza kuwa wananchi wote wanapaswa kuelewa kuwa hata wakati wa uchaguzi Serikali bado inakuwa macho, hivyo wazingatie sheria na taratibu.

“Nawasihi wagombea kuepuka matusi na vurugu, tumtangulize Mungu katika kampeni zetu, matusi na kejeli hayajengi. Kwa yeyote atakayetaka kuleta vurugu wakati wa uchaguzi ninamtahadharisha, Serikali iko macho, Serikali itaendelea kusimamia sheria na taratibu za nchi,” amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewashukuru wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, na kipekee akawashukuru pia wabunge wa vyama vya upinzani kwa ushirikiano wao.

“Nawashukuru pia wabunge wa vyama vingine kwa ushirikiano wao. Japo walikuwepo wale ambao kila jambo walikuwa wanapinga, lakini nao nawashukuru, naamini wakati ujao watakuwa wamejifunza kuwa kupingapinga kila kitu napo sio vizuri,” amesema.

Bunge la la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililodumu mwa kipindi cha miaka mitano limevunjwa rasmi leo. Wabunge wanarejea kutafuta tena nafasi kupitia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya Urais kwa vyama vya upinzani umeanza, wakati kwa chama tawala hali inaonesha dhahiri kuwa Rais Magufuli atapitishwa na chama chake bila kupinga.

Kwa upande wa Zanzibar, tayari wanasiasa wameshajitokeza kuchukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.

JPM atahadharisha kampeni za matusi, awashukuru wapinzani

Ummy akemea matumizi mabaya ya simu kwa watoto “huchochea ngono”

Morrison kurudi kundini kwa masharti
Aubameyang aonyesha matumaini Arsenal