Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kujiepusha na masalia ya fikra za kikoloni za kuamini watawala wa zamani wa Afrika ndiyo wenye uwezo wa kusaidia kuendeleza rasilimali za Afrika.

Ameyasema hayo jana 29 Agosti, 2019 Ikulu Jijini Dar es salaam, alipokuwa akihutubia mkutano wa 6 wa Jukwaa la Uongozi Afrika unaohudhuriwa na Marais Wastaafu, Benjamin William Mkapa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Hassan Mohamud (Somalia).

Amesema kuwa maana hasa ya kupigania uhuru ilikuwa ni kurejesha rasilimali, lakini pia kuwa na maamuzi kamili kuhusu namna ya kuzisimamia na kuzitumia kwa manufaa ya wananchi, ili kuleta ukombozi wa kiuchumi, ambapo hiyo ndiyo ilikuwa maana pekee ya kulinda uhuru wa kisiasa.

“Tusijidanganye watawala wetu wa zamani hawawezi kugeuka kwa usiku mmoja na kuwa wajomba zetu au wakombozi wetu kiuchumi, utegemezi huu ndio umeimarisha mizizi na misingi ya ukoloni mamboleo, ni lazima tuamke,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ametaja sababu ya pili inayosababisha usimamizi mbaya wa rasilimali za Bara la Afrika, kuwa ni tafsiri potofu ya msingi wa maendeleo, kwa kudhani fedha ni msingi wa maendeleo hali iliyosababisha viongozi wake kuzunguka katika Mataifa tajiri kuomba misaada na mikopo.

Magari 20 ya wizi kutoka Kenya yakamatwa Tanzania
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 30, 2019