Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kufuatia kifo cha msanii mkongwe hapa nchini Mzee Amri Athuman maarufu kwa jina la ‘King Majuto’ kilichotokea tarehe 8/8/2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es salaam.

Katika salamu hizo Rais Dkt. Magufuli amemtaka waziri Dkt. Mwakyembe kufikisha salamu za pole kwa familia ya marehemu, wasanii wote nchini, wadau wa sanaa, ndugu jamaa na marafiki na wote walioguswa na kifo cha King Majuto.

Aidha, Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na serikali kuhimiza maendeleo.

“King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali ya juu  katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake wakati wote wa uhai wake,”amesema Rais Dkt. Magufuli

Hata hivyo, Rais Dkt. Magufuli ameongeza kuwa anaungana na familia na wote walioguswa na kifo cha King Majuto katika kipindi hiki cha majonzi na anamuombea kwa mwenyezi Mungu apumzike mahali pema peponi.

Safari ya mwisho ya Mzee Majuto kuagwa leo Dar, kuzikwa kesho Tanga
Ridhiwani, Idris, Wema Sepetu na Zamaradi wamlilia Mzee Majuto, wameandika haya