Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesisitiza kuwa atahakikisha anatumia kipindi kilichowekwa kikatiba kukaa madarakani.

Akizungumza leo jijini Dodoma alipokuwa anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa takribani kilometa 50, katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma; na kuzindua Jengo la Ofisi ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Magufuli amesema kuwa kazi ya Urais ni ngumu na inahitaji maombi.  

“Nataka niwahakikishie pia kuwa kazi hii ni ngumu sana, ina mateso sana. Inahitaji sala, inahitaji nguvu za Mwenyezi Mungu. Kwenye hilo ndugu zangu muendelee kuniombea,” amesema Rais Magufuli.

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wiki hiii walieleza nia yao ya kumuomba au hata kumlazimisha Rais Magufuli kuongeza muda wa kukaa madarakani, hata baada ya kumaliza mihula miwili iliyowekwa na Katiba iliyopo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy kutunza hoja hiyo  hadi watakaporejea tena kwa Bunge la 12, baada ya uchaguzi Mkuu, na kwamba kuna uwezekano wa kuwasilisha Bungeni hoja ya kubadili kipengele cha Katiba na kumuongezea muda Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewapongeza Watanzania kwa jinsi walivyoweza kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Aliwataka kuendelea kuimarisha tiba asilia kwani ni tiba kama zilivyo tiba za aina nyingine ya dawa za kigeni. Hivyo, aliagiza kitengo cha Tiba Asili Muhimbili kiwezeshwe zaidi.

“Tusidharau dawa za kienyeji hata kidogo, uchawi tu ndio mbaya. Ndio maana miti hii yote iliumbwa na mwenyezi Mungu. Ndio maana kile kitengo cha Muhimbili cha Tiba asili nimeagiza kiendelezwe, kiongezewe bajeti ili kifanye kazi nzuri zaidi,” amesema Rais Magufuli

“Tulipumbazwa kwamba tusiamini kilicho chetu, tuamini kilicho chetu. Kama wewe unadhani dawa za kienyeji zimepitwa na wakati, wewe ndiye umepitwa na wakati,” ameongeza.  

Rais Magufuli pia aligawa pikipiki kwa maafisa Tarafa, ili ziwasaidie katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.

Vingozi wa vijiji matatani baada ya polisi kukamata hekari 100 za bangi

FC Bayern Munich Vs Bayer 04 Leverkusen fainali DFB-Pokal

Bajeti 2020 / 21: ukuaji pato la Taifa kushuka, deni lafikia Trilioni 55.43
FC Bayern Munich Vs Bayer 04 Leverkusen fainali DFB-Pokal