Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka viongozi wote waliotajwa katika ripoti ya kamati ya uchunguzi wa madini ya Almasi na Tanzanite kujiwajibisha wenyewe kabla hajawachukuliwa hatua.

Ameyasema hayo mapema hii leo Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite uliofanywa na kamati mbili za bunge zilizoundwa na Spika Job Ndugai.

Amesema kuwa kama mtu anatajwa tajwa kila sehemu basi lazima kuna kitu, kwani kamati hizo haziwezi kumuonea mtu, wala spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano haliwezi kumuonea mtu yeyote.

Aidha, pamoja na kuwataka kuachia ngazi wenyewe, pia amevitaka vyombo vya usalama vyote nchini kuwachukulia hatua mara moja ili waweze kuwajibika kufuatia makosa waliyoyafanya.

“Kuna watu ambao wanatajwa kila sehemu, ukienda huku wapo, kule wapo, ingawa siwezi kuingilia mamlaka ya bunge lakini Spika kama mnaguswa mnapaswa kuwashughulikia watu hao,”amesema Rais Dkt. Magufuli

Vile vile, Rais Dkt. Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama viwafuatilie wale wote waliotajwa katika ripoti hiyo ambao ni wateule wake ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.

Hata hivyo, katika ripoti hiyo mawaziri waliotajwa ni pamoja na waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandis Edwin Ngonyani, pamoja na wale wa zamani ambao ni Sospeter Muhongo na William Ngeleja.

Waziri Simbachawene ajiuzulu
Sentensi 10 za JPM baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa Tanzanite, Almasi (+Video)