Baada ya kufanikiwa kufuzu kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kuifunga Hoffenheim juma la mabao 6 kwa 3, meneja wa Liverpool Juergen Klopp, ameahidi kutumia nafasi hiyo kukiongezea nguvu kikosi chake kabla ya dirisha la usajili halijafungwa juma lijalo.

Liverpool waliikandamiza Hoffenheim mabao 4 kwa 2 usiku wa kuamkia leo katika mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa Anfiled. Ushindi ambao ulitanguliwa na ule wa mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa juma lililopita nchini Ujerumani  na kumalizika kwa ushindi wa mabao 2 kwa 1.

Wapinzani watatu wa Liverpool katika hatua ya makundi watajulikana wakati wa hafla ya upangaji wa makundi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya itakayofanyika mjini Nyon nchini Uswiz.

“Ni hatua nzuri tuliyofikia, sina budi kujipanga kufanya usajili ili kikosi chetu kiwe na nguvu ya kutosha ya kupambana kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya,” Alisema Klopp katika mkutano na waandishi wa habari.

“Kama unazungumzia wachezaji wa kusajiliwa, wapo, na mimi ninawajua kutokana na orodha yangu kuonyesha idadi nitakayoiongeza kikosini.”

Klabu hiyo ya Merseyside tayari imeshamsajili mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Misri Mohamed Salah, ambaye alikua AS Roma. Liverpool pia ilimsajili beki Andrew Robertson na mshambuliaji Dominic Solanke.

Kikosi cha Liverpool kwa sasa kinaelekezea nguvu kwenye mchezo wa ligi ya nchini England, utakaowakutanisha na Arsenal siku ya jumapili kwenye uwanja wa Anfield.

FC Barcelona Yawinda Watatu Ujerumani
Korea Kaskazini yazidi kuivuruga Marekani.