Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Mbarala Maharagande amesema kuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro amekamatwa na Polisi jana Julai 5, 2018 na hadi sasa anashikiliwa na polisi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema Mtatiro amekamatwa kutokana na ujumbe alioutuma katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook unaodaiwa kumkejeli Rais Magufuli.

“Juzi Mtatiro alipokea simu ya wito wa kuhitajika kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam. Jana alikuwa amealikwa kama mmoja wa wageni wawezeshaji wa mjadala na taasisi ya Twaweza katika kongamano la kujadili maoni ya wananchi kuhusu kushiriki maandamano na siasa,” amesema Maharagande.

Maharagande amesema Mtatiro wakati akiwa njiani kuelekea katika mwaliko huo, alipigiwa simu kujulishwa afike kituoni hapo saa nne asubuhi.

Amesema aliambatana naye mpaka kituoni hapo na walipokelewa na ZCO na kujulishwa kuwa anahitajika achukuliwe maelezo yake kuhusu ujumbe alioutuma katika mtandao huo.

“Tukakabidhiwa maofisa wa polisi wa kufanya kazi hiyo. Wakati wa kuanza kuchukuliwa maelezo yake alielezwa kuwa anatuhumiwa kwa kutuma ujumbe wa kejeli na kashfa dhidi ya Rais Magufuli kupitia mtandao wa kijamii.”

Amebainisha kuwa mwenyekiti huyu wa CUF upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alichukuliwa maelezo hadi saa 10 jioni, baadaye kuelekea nyumbani kwake kwa upekuzi.

Baada ya upekuzi huo, Maharagande amesema kuwa walirejea tena kituoni hapo saa 4 usiku na maofisa wa polisi walimueleza kuwa wataendelea kuwa naye mpaka leo asubuhi,

“Walisema watatujulisha kama watampatia dhamana au vinginevyo.” amesema Maharagande, kwa mujibu wa taarifa ya Mwananchi.

Moto wa Lugola wamchoma Kamishna Magereza, amtimua
Brazil kumkosa Danilo kwenye kombe la dunia

Comments

comments