Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Raadhan Mgunda amesema, hatotaka mzaha kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 64 Bora, hivyo atashusha kikosi kamili.

Simba SC itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kesho Jumamosi (Desemba 10), kukabili Eagle FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.

Mgunda amesema katika soka la sasa hakuna timu ndogo, hivyo kikosi chake kitajiandaa vizuri kukabili Eagle FC ambayo kwa mara ya kwanza itakutana na Simba SC katika historia ya Soka la Tanzania.

Kocha huyo mzawa amesema anahitaji kuanza kampeni ya kuwania Taji la ‘ASFC’ linaloshikiliwa watani zao wa jadi Young Africans, kwa kishindo na hilo linawezekana, endapo wachezaji wake watakuwa makini wakati wote wa mchezo.

“Tunajiandaa kuanza vizuri Michuano hii, tunahitaji kushinda ili tusonge mbele, hautakuwa mchezo rahisi kwani michezo yote ni migumu na ya ushindani kulingana na aina mpinzani unayekutana naye,” amesema Mgunda

Kocha huyo amesema malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanafanya vizuri na kurejesha mataji yote waliyoyapoteza msimu uliopita na hilo kila mchezaji wake analifahamu.

“Tumerudi kwenye Uwanja wa mazoezi ili kujiimarisha, tutapambana katika mchezo huo kwa tahadhari kubwa, kwa sababu hakuna timu ambayo ni dhaifu, ukifika hatua hii basi wewe ni bora, timu za madaraja ya chini husumbua timu kubwa.”

Katika hatua nyingine Kocha Mgunda amesema amafurahi kuona mchezaji wake Nelson Okwa amerejea kutoka nchini kwao Nigeria alipokwenda kwa ajili ya matibabu, na ujio wake umemuongezea kufanya chaguo kwenye kupanga kikosi.

Azam FC watofautiana usajili wa Fei Toto
Azam FC yatangaza vita na Young Africans