Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wataalamu wa maji kutumia taaluma zao vizuri, na kuacha tabia ya kuwadanganya viongozi pindi wanatofuatilia miradi katika maeneo yao  ya kazi kuwa miradi hiyo iko vizuri hali kwamba kuna kasoro katika miradi hiyo.

Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha wadau wa Maji, Wakurugenzi, wakuu wa mamlaka za maji na wenyeviti wa bodi za maji waliokaa kwa siku mbili Dodoma kupewa uelewa namna ya utekelezaji wa sheria mpya ya maji na usafi wa mazingira, pamoja na uanzishwaji wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini.

Amesema kuwa wataalamu hao wamekuwa wakitumia taaluma zao vibaya katika nafasi zao na kufikia kipindi kuwadanganya viongozi kuwa hakuna shida kwenye miradi ya maji mbalimbali, lakini ukifuatilia kwa undani unakuta kuna matatizo mengi na wananchi hawapati maji.

“Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wataalamu wetu kwa sababu tukifika kukagua miradi ya maji tunaambiwa miradi iko vizuri lakini ikiikagua kwa umakini unakuta kuna matatizo makubwa, tabia hii muache natumaini kupitia kikao hiki mtakuwa mmejifunza mengi,”amesema Aweso.

Aidha, amesema hata sita kumfukuza kiongozi yeyote ndani ya mamlaka hiyo ambaye atakwenda kinyume na maelekezo yao, japo hakuna mtu anayependa kumfukuza mtu katika kazi yake.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Idara ya utawala wizara ya maji, Barnabas Ndunguru aliyekuwa akimuwakilisha katibu mkuu, amesema watatumia taaluma zao kuhakikisha wanashirikiana na wizara kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa ufasaha na hasa katika kutekeleza majukumu ya mamlaka mpya ya maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA.

Naye afisa maji bonde la ziwa Nyasa, Alice Mnali amesema kuwa watahakikisha wanalinda taaluma zao kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na kuleta anufaa katika jamii, na yale yote waliopata katika mawasilisho mbalimbali watahakikisha wanayatendea kazi, na hawatakuwa kikwazo katika sekta ya maji.

Video: Aliyosema Kibonde kuashiria kifo chake, Kamwene Mbowe na Matiko
Mbunge amwaga fedha ujenzi wa vyumba vya madarasa