Wakristo karibu wote kote ulimwenguni leeo wanaanza kipindi cha Kwaresma ambacho huanza siku ya Jumatano ya Majivu. Je, unafahamu maana halisi ya Jumatano ya majivu na ni kwa nini hupakwa majivu?

Jina la Jumatano ya Majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbani II: mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Majivu yatumikayo hutokana na matawi yaliyobarikiwa Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita. Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni wakati wa kumwilisha utamaduni wa Injili ya upendo!

Kipindi cha Kwaresima huanza na jumatano ya majivu na hudumu kwa muda wa siku 40 mpaka siku inayotangulia siku tatu kuu zinazotangulia Pasaka; yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana Yesu Kristo.

Katika kipindi hiki, wakristo wanaalikwa kutafakari sana fumbo la wokovu wa Kristo na kuishi ubatizo wao kwa undani kabisa.

Ni siku 40 za utakaso ambazo Wakristo wanakumbuka siku 40 alizokaa Yesu jangwani akisali na kufunga kabla ya kuanza utume wake.

Wakristo huungana kufuata njia ya msalaba, ile ya Kalvari, wakitafakari kwa kina maana ya imani yao na kuishi katika matendo kile wanachokiamini.

Biblia Takatifu katika kitabu cha Mwanzo 3: 19 inaandikwa; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa, kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. 

Siku ya Jumatano ya majivu Wakristo hupakwa majivu utosini au kisogoni.

Je, Maana yake nini? Kupitia tovuti ya Vatican News Padre Reginald Mrosso  anaeleza kuwa, “Alama hii yatukumbusha kuwa mwili wa mwanadamu u katika hali ya uharibifu na ukomo. Alama hii ikituelekeza kwenye matumaini makuu. Tunaishi tukitambua kuwa sisi si kitu na ulimwengu huu ni mahali pa kupita tu. Tunakiri na kukubali waziwazi mbele ya Mungu Baba Muumba wetu na mbele ya wenzetu kuwa sisi tumepungukiwa. Ni majivu tu. Lakini huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Tunakiri dhambi zetu. Mtu mmoja anafanya tafakari hii: majivu ni masalio ya moto, makazi yake jalalani. Ila yakisugua sufuria yenye masizi huifanya kuwa nyeupe pe. Japo tu dhaifu, tuna thamani zaidi ya majivu.

“Alama ya pili ni sauti ya Yesu. Katika kitabu cha Marko 1:16  tunasoma – tubuni na kuiamini Injili. Na hapa Yesu anaanza safari yake ya kitume na unakuwa mwaliko kwetu, mwaliko wa kuelekeza matumaini yetu katika Neno la Mungu. Kipindi hiki kama tulivyosikia hapo juu – tunaalikwa kuwa karibu zaidi na Neno la Mungu kwa imani na matendo. Maisha ya mkristo ni maisha ya imani, yenye msingi wake katika Neno la Mungu – na anayelishwa na Neno la Mungu anao uzima wa milele. Njia kuu ya kushinda vishawishi na dhambi ni kusikiliza Neno la Mungu – ili kuwa na uwezo wa kukataa vishawishi vya shetani,” amaandika   Padre Reginald Mrosso.

Wakristo wanapofunga hutakiwa kuzuia vilema vyao na kuviacha kabisa, kuomba kujaliwa moyo wa toba, kuinua mioyo na kumuomba Mungu awajalie nguvu na tuzo.

Katika kipindi cha Kwaresma Wakristo hutakiwa kufunga, kusali na kutenda matendo ya huruma.

Padre Reginald Mrosso anafanua mambo haya katika andiko lake lifuatalo.

SALA: Kwa kifupi kusali kwa mkristo maana yake ni kuruhusu upendo wa Mungu utawale ndani ya mioyo yetu na hivyo kuwa katika mwelekeo wa kusikiliza sauti za ndani ya mioyo ya mwanadamu na kujiweka mbele yake na vyote tulivyo navyo. Kusali kwa mkristo ni kuishi maisha ya sala kama sadaka na sifa kwa Mungu Muumba wetu. Sala pia inatuunganisha na Yesu, kanisa na historia yake kwa ujumla na inatusaidia kufunua mioyo yetu mbele ya Roho Mtakatifu ambaye anafanya kila kitu kuwa kipya. Kwa ufupi sala katika utatu Mtakatifu ndiyo jambo ambalo kila mwanadamu anapaswa kulitambua na kuligundua kipindi hiki.

KUFUNGA: Kufunga kwa asili ya kiroho ina maana kubwa katika elimu ya mambo ya mwisho hasa inapotokea kuwa kuna jambo kubwa linalosubiriwa. Ni kama vile mahitaji ya mwanadamu ya kula yanashika nafasi ya pili kwa vile mwanadamu analishwa na hamu hiyo na matarajio hayo. Hicho ndicho chakula chake. Utamaduni wa kikristo wa kufunga unawakilisha zaidi ya yote ukomo wa matarajio ya kumngoja bwana na kufungua mioyo yao, na kujinyima kwa kila kitu ambacho kinaonekana kuwa ni kikwazo kuwa karibu na Mungu. Ni kungojea kwa hamu kubwa, chukua mfano wa mtu anayeshinda njaa akipata chakula atakavyokifurahia. Kwa kufunga tunatengeneza nguvu za kutawala miili yetu, vionjo vyetu n.k.

Kwa kufunga tunakuwa na uwezo wa kuiambia miili yetu kile tutakacho kufanya. Mfano tunajinyima chakula fulani kitamu, kizuri au kitu kitamu na kizuri tukipendacho na katika kujinyima huko tunatoa msaada au kujinyima huko tunawasaidia wengine ili nao washiriki nasi upendo huo. Au kwa kutoendeleza mapenzi yetu  tu, tukijinyima kufanya hilo tulipendalo tunapata muda wa kufanya jambo fulani jema kwa ajili ya wengine. Na hapa wakristo wanaalikwa kuwa makini – huwezi kufunga na kufaidi tena hicho hicho unachopenda kukiacha. Kwa tendo la kufunga tunapata uwezo wa kuiambia miili yetu kile tupendacho kufanya na si miili yetu ituambie kile cha kufanya. Kwa maana hiyo basi, kufunga kunamaanisha ni hija kuelekea kipindi cha pasaka na hivyo mwanadamu anapaswa kutambua kuwa tunamhitaji Mungu kama chanzo cha uwepo wetu na pia kujiweka wazi ili Mungu aweze kuwa ndani yetu.

MATENDO YA HURUMA – KUTOA SADAKA: Matoleo mengineyo mema zaidi ya utoaji wa sadaka pia ni mwelekeo wa moyo. Moyo ambao ni mpole, wa toba, wenye huruma na wa faraja ambao unatafuta mahusiano na wengine katika kuhurumia wengine ili kukuza mahusiano na Mungu. Kwa hiyo au sadaka yaonesha kujali, kufanya kitu halisi, zawadi ambayo waamini wanatoa wanapojaribu kuwazia upendo wa Mungu ambao unawakubali na kuwasamehe. Je Mungu ametujalia mambo mangapi mema? Sisi tumemrudishia nini? Kwa asili na maana ya kutoa sadaka ni kupoteza pia. Huwezi kutoa sadaka na kutarajia hapo hapo kufaidi yote pia. Mfano mzuri ni Bwana wetu Yesu Kristu – alitoa uhai wake kwa ajili yetu. Hii ndiyo changamoto iliyo mbele yetu leo hii. Ni wangapi tuko tayari kutoa sadaka kwa ajili ya wengine? Kujitoa kweli kwa hali na mali? Bila manung’uniko. Bila kudai faida?

“Hakika kipindi hiki cha Kwaresima ni muda wa kuangalia upya thamani ya sadaka ndogo, alama ya upendo, inayotolewa kwa unyenyekevu, kwa siri na ambayo ni halali, ambayo inakugharimu, na inafanywa katika kumtukuza Mungu katika wale wanaotaabika, na wahitaji. Tukijenga tabia au mazoea ya kutoa kwa ajili ya wahitaji tunajenga pia mazoea ya kuwa huru na mambo ya dunia hii yanayopita. Kila mmoja wetu ana hitaji fulani katika maisha yake, hakuna tajiri kabisa kwamba hana cha kupokea au maskini sana kwamba hana cha kutoa. Kutoa ni moyo na si utajiri,” anaandika Padre Reginald Mrosso.

Dar24 inawatakia Wakristo wote mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima na mfungo mwema.

Tanzia: Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif afariki dunia, Rais Magufuli amlilia
TCRA yatoa siku 90 kwa makampuni ya simu