Shirikisho la soka nchini Marakani (USSF) limechukua maamuzi ya kumtimua kazi kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Jurgen Klinsmann, kufuatia matokeo mabaya aliyoyapata katika michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia ukanda wa Amerika ya kati na kaskazini (CONCACAF).

Rais wa USSF Sunil Gulati alizungumza na vyombo vya habari na kuthibitisha kutimuliwa ka Klinsmann aliedumu katika ajira ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Marekani kwa miaka mitano.

Gulati alisema maamuzi ya kutimuliwa kwa kocha huyo kutoka nchini Ujerumani, yamefikiwa baada ya kuzungumza nae na kukubaliana baadhi ya mambo ya kimsingi zikiwepo haki zake ambazo zinapaswa kulipwa kwa wakati maalum.

Alisema wameona ni bora kuachana na Klinsman na kuanza kusaka mtu mwingine ambaye atakua na uwajibikaji wa kufanikisha azma ya kuifikisha timu ya taifa ya Marekani katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, ambazo zitafanyika nchini Urusi.

Marekani walishindwa kupata ushindi katika michezo miwili ya kufuzu fainali hizo juma moja na nusu lililopta kwa kufungwa na Costa Rica na kisha kutoka sare ya bila kufungana na Mexico.

Costa Rica waliifunga Marekani mabao manne kwa sifuri (4-0) na kulifanya taifa hilo lenye nguvu za kiuchumi duniani kuendelea kubaki mkiani mwa kundi la ukanda wa CONCACAF.

Hali hiyo imeiweka Marekani katika hatari ya kudhaniwa huenda ikazikosa fainali za kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1986.

Hata hivyo bado nchi hiyo ina nafasi kubwa ya kujiondoa kwenye janga hilo, kufuatia kusaliwa na michezo dhidi ya wapinzani wake ambayo itacheza katika mfumo wa nyumbani na ugenini.

Timu ambazo zimeingia katika hatua ya mwisho ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018 ukanda wa CONCACAF ni Mexico, Honduras, Panama, Trinidad na Tobago, Costa Rica na Marekani.

Yametimia, Hector Bellerin Kubaki Arsenal FC
Jack Wilshere Akata Tamaa, Adhamiria Kuondoka Jumla