Kiungo mshambuliaji Adam David Lallana anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha majogoo wa jiji Liverpool, ambacho kesho kitakau na shughuli ya kuwania nafasi ya kucheza fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya AS Roma.

Lallana anapewa nafasi kubwa ya kucheza mchezo huo, kufuatia kupona kabisa majeraha ya goti, na tayari jopo na madaktari limethibitisha utimamu wake wa mwili, baada ya kufanya mazoezi ya pekee yake kwa majuma kadhaa na baadae kujiunga na wenzake.

Lallana ambaye alisajiliwa na Liverpool mwaka 2014 akitokea Southampton, hajacheza soka tangu mwezi Machi mwaka huu, baada ya kuumia katika mchezo wa ligi dhidi ya Crystal Palace.

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amethibitisha kiungo huyo ni miongoni mwa wachezaji 23 wa kikosi chake waliosafiri leo kuelekea mjini Roma, tayari kwa mpambano wa kesho.

Hata hivyo Liverpool itaendelea kumkosa Alex Oxlade-Chamberlain ambaye alipata majeraha ya goti katika mchezo wa mkondo wa kwanza mjini Liverpool pamoja na kiungo Emre Can anaesumbuliwa na majeraha ya mgongo.

Naye beki Joe Gomez amelazimika kubaki mjini Liverpool, baada ya kupata maumivu ya kifundo cha mguu wakati wa mchezo wa ligi mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Stoke City, ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Kwa upande wa mshambuliaji Sadio Mane, ambaye hakucheza dhidi ya Stoke City mwishoni mwa juma lililopita, amesafiri na kikosi hii leo sambamba na wachezaji wengine ambao walikua mashakani kuukosa mchezo dhidi ya AS Roma Jordan Henderson na beki Trent Alexander-Arnold ambao wamepita katika vipimo vya afya.

Liverpool itakua na kazi ya kulinda ushindi wake wa mabao matano kwa mawili walioupata katika mchezo wa mkondo wa kwanza juma lililopita, huku AS Roma ambao kesho watakua nyumbani uwanja wa Olimpico watahitaji kupindua matokeo hayo kama walivyofanya kwa FC Barcelona.

AS Roma watalazimika kusaka ushindi wa mabao matatu kwa sifuri na kuendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu.

Eusebio Di Francesco: Tutaishangaza tena dunia
Mohamed Salah Ghaly mchezaji bora F.W.A