Majogoo wa jiji Liverpool, hii leo watakabiliwa na shughuli ya kuwania ubingwa wa Europa league kwa kupambana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Sevilla CF kutoka nchini Hispania.

Liverpool wamefikia hatua ya kucheza hatua hiyo kubwa kwa msimu huu, chini ya utawala wa meneja kutoka nchini Ujerumani, Jurgen Klopp na mashabiki wengi wanatoa nafasi kwao kufikia lengo ya kutwaa ubingwa huo, kutokana na kuwa na historia nzuri katika michuano ya barani Ulaya.

Hata hivyo wapo baadhi ambao hawaamini kama Liverpool wanaweza kufikia lengo hilo, kutokana na utayari wa wapinzani wao ambao watakua wanahitaji kutwaa ubingwa wa Europa league kwa mara ya tatu mfululizo.

Alipoulizwa meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp kuhusu nafasi kubwa anayopewa ya kuiwezesha The Reds kutwaa ubingwa wa barani Ulaya hii leo, alisema hana uhakika kama hilo litafanikiwa kirahisi.

Alisema kikosi chake kipo tayari kupambana kwa wakati wote, na lengo ni kushinda lakini akagusia upande wa wapinzani wapinzani wake, kwa kusisitiza maandalizi yao ambayo anaamini yamekwenda vyema kwama ilivyo kwa Liverpool.

Hata hivyo meneja huyo ambaye alipita kwenye klabu ya Borussia Dortmund na kupata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa nchini Ujerumani pamoja na kucheza hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2012-13, amebainisha kuwa katika maisha yake hakuwahi kujifunza na kuliamini neno “Kushindwa”.

“Katika maisha yangu sijawahi kukubali ama kuamini kama kuna jambo linaitwa kushindwa, na hatua hiyo imekua ikinisaidia katika kila hatua ninayoipiga.

“Kama utafuatilia utendaji wangu wa kazi, nimekua na kasumba ya kupambana hadi katika mchezo wa mwisho, na hata ikitokea ninapoteza huwa naamini nimepambana kweli kweli

“Ninajua hii ni bahati ilioje kwetu sisi (Liverpool) na hatuna budi kuitendea haki kwa kupambana bila uwoga.

“Unaweza kusema ni bora ungetolewa katika hatua ya nusu fainali, pale inapojitokeza unapoteza mpambano wa fainali, lakini kwangu ninaamini majuto hayo hayatokuwepo.” Alisema Klopp alipozungumza na vyombo vya habari mjini Basel nchini Uswiz.

Tayari Liverpool wameshawasili mjini Basel, siku mbili zilizopita sambamba na Sevilla CF.

NEW VIDO: ALICIOS ft. KIDUM - PETE (OFFICIAL 4k VIDEO)
Yondani Amrudisha Nadir Haroub Taifa Stars