Meneja wa majogoo wa jiji (Liverpool), Jurgen Klopp amekosoa mpango wa baadhi ya klabu za soka nchini England pamoja na nchi nyingine za barani Ulaya wa kufanya usajili kwa kutumia pesa nyingi kwa mchezo mmoja.

Klopp amepinga mpango huo kwa kusema hawezi kufanya kitu kama hicho katika falsafa zake za soka anazozitumia kila napokua ofisini, na badala yake amejipanga kufanya jambo tofauti katika harakati za usajili akiwa na klabu ya Liverpool.

Klopp amekosoa mpango huo, huku mahasimu wake Man Utd wakiwa katika mchakato wa kutaka kukamilisha dili la usajili wa kiungo kutoka nchini Ufaransa na klabu bingwa nchini Italia Juventus FC, Paul Pogba ambalo litawagharimu kiasi cha Pauni milioni 100.

Akifanyia mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha ESPN kilichopo nchini Marekani, meneja huyo kutoka nchini Ujerumani, alisema huenda ikawa hasara kubwa kwa klabu inayotumia mfumo wa kutumia pesa nyingi kwa mchezaji mmoja, pale inapotokea anaumia ama anacheza chini ya kiwango na ilivyotarajiwa.

“Kama unamsajili mchezaji kwa ada ya Pauni milioni 100, na ikitokea anapata majeraha, ama anacheza chini ya kiwango hiyo inakua ni hasara kubwa kwa klabu,” Alisema Klopp.

“Mchezo wa soka unatakiwa kubadilika siku hadi siku kutokana na mazingira yaliopo, hivyo unapaswa kuwa muangalifu na mbunifu katika matumizi ya pesa za usajili wa wachezaji, kwani jambo hilo ndio linatoa mustakabali mzima wa msimu wako wa ligi.

Alisema anajitahidi kutumia pesa katika mfumo mzuri kwa kuwasajili wachezaji wenye thamani ya kawaida ili aweze kuipa faida klabu ya Liverpool na ndio maana ameona umuhimu wa kuwa na mshambuliaji kutoka nchini Senegal, Sadio Mane ambaye alimsajili akitokea Southampton, kwa ada ya Pauni milion 34 pamoja na Georginio Wijnaldum aliyetokea Newcastle United kwa kiasi cha Pauni milion 23, sambamba na Joel Matip na Loris Karius.

Klopp sambamba na kikosi chake kwa sasa wapo nchini Marekani wakijiandaa na msimu mpya wa ligi ya nchini England kwa kushiriki michuano ya International Champions Cup (ICC), na mchezo ujao watacheza dhidi ya AC Milan katika uwanja wa Levi uliopo katika kitongoji cha Santa Clara jimbo la California.

Gonzalo Higuain Afichua Siri Ya Kuondoka SSC Napoli
Pep Guardiola Asisitiza Usajili Wa Leroy Sane, John Stones.