Meneja wa klabu ya Liverpool Jurgen Klopp amesema hawana wa kumlaumu zaidi ya kujilaumu wao wenyewe kwa kushindwa kupata point tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Anfield, ambapo walikutana na mahasimu wao Man Utd usiku wa kuamkia hii leo.

Akiwa katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mpambano huo kumalizika, Klopp alisema walipaswa kushinda mchezo huo kutokana na maandalizi mazuri waliyokua wameyafanya, lakini kwa bahati mbaya wachezaji wake walishindwa kuzitumia nafasi walizozitengeneza dhidi ya wapinzani wao.

Alisema kwa hakika wachezaji wake walionyesha jitihada za kupambana, lakini hawakufikia lengo la kumfurahisha yeye kama meneja pamoja na mashabiki waliokua wanasubiri ladha ya ushindi.

Hata hivyo meneja huyo kutoka nchini Ujerumani alishindwa kujizuia na kujikuita akimwagia sifa kedekede mlinda mlango wa Man Utd David de Gea, ambaye alijitahidi wakati wote huku akiokoa michomo ya hatari iliyoelekezwa langoni mwake na Emre Can na Philippe Coutinho.

“Sikufurahishwa na tulivyocheza. Kwa hakika ulikua mchezo wenye mitihani mingi. Ulikua na shinikizo. Sidhani kama tulicheza kama tulivyokua tumejipanga kucheza dhidi ya Man Utd.

“Tulianza vizuri, lakini umakini wa wapinzani wetu wa kukaba mtu na mtu nao ulichangia tushindwe kufikia lengo la kumaliza mchezo tukiwa wenye furaha. Japo ilikua hivyo, bado tulitengeneza nafasi kadhaa lakini tulishindwa kuzitumia

“Nakumbuka tulikuwa na nafasi mbili ama tatu ambazo zilipaswa kutupa ushindi, lakini umahiri wa David de Gea, ulituharibia mipango ya kumaliza tukiwa katika hali nzuri kwa kuzipata point zote tatu.

Kwa matokeo hayo Liverpool wamefikisha point 17 ambazo zinaendelea kuwaweka katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya nchini Uingereza na kwa wapinzani wao Man Utd wamefikisha point 14 na kusalia kwenye nafasi ya saba.

Neymar Kuandika Rekodi Mpya FC Barcelona
Mbunge adaiwa kutafuna mishahara mitano ya utumishi hewa