Klabu ya Soka ya Italia, Juventus imevunja ukimya kuhusu tetesi za kutaka kumvuta tena mshambuliaji anayekipiga Manchester United, Paul Pogba katika dirisha la usajili.

Tetesi za Pogba kurejea Juventus zilivuma zaidi wakati Jose Mourinho akiwa kocha wa Wekundu hao wa Old Trafford, lakini zilianza kupungua baada ya Ole Gunnar Solskjaer kushika usukani akimpa nafasi ya kutosha mshambuliaji huyo kutoka Ufaransa.

Kiwango bora zaidi kilichooneshwa na Pogba katika wiki za hivi karibuni kimemuibua Meneja wa Juve, Massimiliano Allegri ambaye amedai kuwa matumaini ya kumnasa tena mshambuliaji huyo yamefifia.

“Ni vigumu sana kumuona Pogba akiichezea Juventus tena,” Allegri aliwaambia waandishi wa habari jana.

“Waandishi wa habari… sitaki kujidanganya [katika hilo]. Nadhani itakuwa vigumu sana kumuona Pogba akiwa ndani ya jezi ya Juventus,” aliongeza.

Pogba alihamia Manchester United mwaka 2016 akitokea Juventus kwa dau la $117 Milioni lililoweka rekodi ya dunia. Aliichezea Juventus tangu mwaka 2012 akiwa kijana mdogo.

Kaka yake, Florentin ameeleza kuwa kama ataondoka Manchester United, Pogba anaweza kuelekea kati ya timu tatu ambazo ni Manchester City, Real Madrid au Barcelona.

Januari 25, Manchester United ilipoichapa Arsenal 3-1, uwezo wa Pogba ulikuwa gumzo mitandaoni. Mwandishi wa habari nguli wa Uingereza, Piers Morgan alichochea moto zaidi baada ya kumfananisha Pogba na Mesut Ozil wa Arsenal anayetajwa kuwa kati ya wachezaji bora zaidi duniani. Wengi hawakukubaliana naye.

TAWIA wamuomba JPM kuanzisha wizara ya wajane
Lissu auweka ubunge wake rehani, kuzuru Ulaya na Marekani