Mwimbaji wa ‘Ntasubiri’, Jux ambaye alinasa kwenye penzi la Vanessa Mdee siku chache baada ya aliyekuwa mpenzi wake, Jackie Cliff kukamatwa na dawa za kulevya nchini China, ameeleza ‘kimtego’ kilichowafanya wawili hao kuzama kwenye penzi zito.

Akiongea na kipindi cha Mkasi, Jux alieleza kuwa alikutana na Vanessa katika studio za B’Hitz zilizoko Kawe Beach jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa akifanya kazi na Mtayarishaji wa muziki, Pancho Latino. Alisema kuwa baada ya kufanya wimbo wake alitamani kuwe na rapa wa kike ndani na ndipo Pancho alipompendekeza Vanessa ingawa awali hakuwa studio.

Jux anasema siku iliyofuata walikutana uso kwa macho na ‘Vee Money’ ndani ya studio hizo na wakati wanaondoka, mrembo huyo alimuomba kumsindikiza nyumbani kwao kwa kuwa hakuwa na gari muda huo.

Jux na Vanessa Mdee 2

Kwa moyo mkunjufu, alikubali na gari hilo walipanda wakiwa na Pancho Latino ambaye aliishia kwake Mbezi Beach. Jux anasema kuwa jicho lake lilikuwa halibanduki kwa Vanessa mara kwa mara na alitumia dakika kadhaa kumuangalia walipokuwa wakikaa pamoja na timu ya wana ‘B’Hitz’ (enzi hizo).

Alisema swali la Vanessa la kutaka kujua kuhusu wimbo wao waliofanya B’Hitz liliwasogeza karibu na kuwapa sababu ya kuzungumza, lakini mtego mmoja tu ulifanikisha kuwazamisha kwenye bahari ya kina kirefu cha mapenzi.

Jux anasema alimuona Vanessa akiwa amevaa ‘kadude’ mkononi C (bracelet), ndipo alipovutiwa na kujita akimuomba ‘kadude’ hako. Hata hivyo ombi lake liligonga mwamba kwani Vanessa alimwambia kana maana sana kwake na ni ‘special’. Lakini kiu ya mwimbaji huyo kumiliki ‘kadude’ hako kutoka kwa Vanessa ilikuwa ya hali ya juu.

Kwa kutambua hilo, Vanessa alipotaka Jux amfuate au wakutane, alikuwa akimuahidi ‘kadude’ hako ili kumvuta afike. “Alikuwa ananiambia ‘njoo basi ufate kale kadude’,” alisema Jux.

Anasema utani huo wa kufuata kadude hako ndio uliopelekea wawili hao kusogeleana na mwisho kujikuta ndani ya penzi zito ambalo chanzo cha Dar24 kimeeleza kuwa lilidumu takribani mwaka mmoja kimyakimya kabla ya kuwekwa hadharani.

 

Dubai Ni Mahala Sahihi Kwa Rooney Kujifariji
Shaba Kuanza Na Hardrock Ligi Kuu Pemba